MWENGE WA UHURU WAFUNGUA FURSA ZA ZABUNI KWA VIJANA KUPITIA NeST

Na Asha Mwakyonde, RUKWA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), taasisi nunuzi na halmashauri nchini kuhakikisha usajili wa vikundi vya vijana katika mifumo ya ununuzi wa umma unaambatana na upatikanaji wa zabuni ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Amesema usajili wa vikundi hivyo hautakuwa na maana endapo vijana hawatapata zabuni, akisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo na kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kushindana na kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali.

Ndejembi ameyasema hayo leo Oktoba 14, 2026, katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kilichofanyika katika Uwanja wa CCM Nelson Mandela, Halmashauri ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha uwezeshaji wa vijana kupitia mitaji na mikopo, ikiwamo programu ya uwezeshaji yenye thamani ya Sh bilioni 200 pamoja na mikopo inayotolewa na halmashauri.

Amesisitiza kuwa mifumo ya Serikali inapaswa kuunganishwa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza fursa kwa vijana, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na Serikali zinawafikia walengwa.

“Na katika hili mifumo yetu ikisomana tutaweza kutoa fursa nyingi zaidi. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari ameonesha njia na sisi kazi yetu ni kuhakikisha mabilioni anayoyatoa kweli yanawafikia vijana ambao wamekusudiwa kufikiwa,” amesema.

Ameongeza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuleta matokeo halisi na yanayopimika katika kuboresha maisha ya vijana kwa kuongeza fursa za ajira, kuwawezesha kujiajiri na kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana), Joel Nanauka, amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2026 zimechangia kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kupitia usajili wa vikundi vyao katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).

Amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha makundi hayo kushiriki katika zabuni za Serikali, kukuza mitaji yao, kujiajiri na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Nanauka amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023, Sura ya 410, kifungu cha 64, inazitaka taasisi nchini kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum yaliyosajiliwa katika mfumo wa NeST.

Ameeleza kuwa kabla ya kampeni ya Mwenge wa Uhuru, kuanzia mwaka 2023 hadi Machi 2026, jumla ya vikundi 1,556 vya makundi maalum vilikuwa vimesajiliwa katika mfumo huo, vikiwamo vikundi 879 vya vijana, 590 vya wanawake, 48 vya wazee na 31 vya watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, amesema katika kipindi cha miezi saba, kuanzia Aprili hadi Oktoba 2026, idadi ya vikundi vilivyosajiliwa iliongezeka na kufikia 33,524.

Amesema kati ya vikundi hivyo, 16,582 ni vya vijana, 15,412 vya wanawake, 789 vya wazee na 741 vya watu wenye ulemavu, hali inayoonesha mwitikio wa makundi hayo katika kutumia fursa zinazotolewa na Serikali.

Aidha, Nanauka amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, mikataba 205 yenye thamani ya Sh bilioni 25.076 ilikuwa imetolewa kwa makundi maalum, hatua inayotarajiwa kuongeza mitaji, kuunda ajira na kupanua masoko ya bidhaa na huduma zao.

Amesisitiza kuwa vijana na makundi mengine maalum wanapaswa kutumia fursa hizo kwa ufanisi ili kujenga uwezo wa kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Katika hatua nyingine, amesema Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2026 umeendelea kuhimiza usikilizaji na utatuzi wa changamoto za vijana kupitia uanzishwaji wa majukwaa ya vijana yatakayowapa nafasi ya kueleza changamoto zao na kushiriki katika kutafuta suluhisho.

Post a Comment

0 Comments

PPRA YANG'ARA KILELE MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026