TANZANIA YASHIRIKI KONGAMANO LA KUIMARISHA USTAHIMILIVU WA MAAFA AFRIKA

Na Mwandishi Wetu, MAPUTO, MSUMBIJI

MABADILIKO ya tabianchi yanayoendelea kuongeza hatari ya ukame, mafuriko, vimbunga na majanga mengine yameongeza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha mifumo ya tahadhari, maandalizi na uwekezaji wa kimkakati ili kupunguza athari kwa maisha ya watu na uchumi wa mataifa hayo.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amewaongoza wajumbe wa Tanzania katika Kongamano la Usimamizi wa Maafa linalolenga kupunguza hatari za majanga na kuimarisha ustahimilivu wa bara la Afrika.

Mmuya ameshiriki kongamano hilo akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, katika mkutano unaofanyika jijini Maputo, Msumbiji, kuanzia Oktoba 13 hadi 15, 2026.

Kongamano hilo limefunguliwa rasmi Oktoba 13 na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, ambaye ameeleza kuwa limefanyika wakati muafaka kutokana na kuongezeka kwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazosababisha majanga mbalimbali katika maeneo tofauti ya dunia.

Ametaja majanga hayo kuwa ni pamoja na ukame, mafuriko, matetemeko ya ardhi na vimbunga vya baharini, akisisitiza umuhimu wa nchi kushirikiana katika kuweka mikakati ya kukabiliana na majanga ya asili na yale yasiyo ya asili.

Chapo amebainisha kuwa ingawa majanga yanaweza kutokea katika maeneo mbalimbali, ukubwa wa madhara yake hutegemea maandalizi, mipango na uwezo wa nchi husika katika kukabiliana nayo.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kuwepo kwa mipango imara ya kiuchumi na kijamii inayowezesha nchi kujiandaa mapema, kupunguza athari za majanga na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na dharura.

Lengo kuu la kongamano hilo ni kuimarisha mifumo ya kiutawala katika usimamizi wa maafa, kuongeza uwekezaji wa kimkakati na kujenga uwezo wa nchi za Afrika kukabiliana na athari za ukame na majanga mengine yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, washiriki wanajadili mikakati ya kugharamia hatua za mapema, kuzuia majanga kabla hayajatokea na kutafuta suluhisho la changamoto za upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kongamano hilo pia linatoa fursa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kujadili namna ya kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano katika usimamizi wa maafa, likiwakutanisha watunga sera, jumuiya za kiuchumi za kikanda, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo, wasomi, sekta binafsi na asasi za kiraia.

Limeandaliwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) kwa kushirikiana na Serikali ya Msumbiji pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), likiwa na kaulimbiu isemayo “Kuimarisha Utawala katika Usimamizi wa Maafa na Uwekezaji wa Kimkakati ili Kupunguza Hatari za Maafa na Kujenga Afrika Imara Inayostahimili Majanga.”
 

Post a Comment

0 Comments

PPRA YANG'ARA KILELE MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026