TFRA YATAKA WAKULIMA KUPIMA AFYA YA UDONGO KUONGEZA MAVUNO


 Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya Mamlaka na Mkulima Sumry katika makazi ya mkulima huyo Nkasi mkoani Rukwa tarehe 13 Oktoba, 2026.

Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Joshua Ng'ondya akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya Mamlaka na Mkulima Salum Sumry mara baada ya kuwasili shambani kwake Msipazi Farm, Nkasi Mkoani Rukwa tarehe 13 Oktoba, 2026.

Mkulima Salum Sumry akizungumza mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA ,Joel Laurent (hayupo pichani) na watumishi alioambatana nao kwenye ziara ya mafunzo shambani kwake Msipazi Farm Nkasi Mkoani Rukwa tarehe 13 Oktoba, 2013.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent (kulia) akisalimiana na Salum Sumry mara baada ya kumtembelea shambani kwake Msipazi Farm, kwa lengo la kujifunza teknolojia mpya za kilimo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mbolea Duniani tarehe 13 Oktoba, 2026.

Na Mwandishi wetu, RUKWA

Wakulima nchini wametakiwa kuzingatia upimaji wa afya ya udongo na matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa mazao na kupunguza gharama za kilimo, hatua inayolenga kukuza kilimo cha biashara na kuongeza tija kwa wakulima.

Wito huo umetolewa wakati wa ziara ya mafunzo iliyofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika Shamba la Sumry, linalofahamika pia kama Msipazi Farm, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, Oktoba 13, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani.

Ziara hiyo iliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, ikiwa na lengo la kujifunza teknolojia mpya za kilimo zinazoweza kuongeza uzalishaji na tija, pamoja na kuimarisha uelewa wa wadau kuhusu mbinu bora za kilimo cha biashara.

Akizungumza na ujumbe huo, Salum Sumry alisisitiza umuhimu wa wakulima kupima afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea, akieleza kuwa matokeo ya vipimo hivyo husaidia kubaini virutubisho vinavyohitajika na udongo pamoja na aina ya zao linalolimwa.

Alieleza kuwa upimaji wa udongo ni hatua muhimu katika kufanya maamuzi sahihi ya kilimo, kwa kuwa humwezesha mkulima kuchagua aina ya mbolea inayofaa kulingana na mahitaji ya udongo na zao husika.

Kupitia ziara hiyo,TFRA imesisitiza umuhimu wa matumizi ya mbolea bora kwa kuzingatia aina ya zao, hatua ya ukuaji na hali ya udongo, ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya pembejeo na kuepuka gharama zisizo za lazima.

Aidha, ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za mamlaka hiyo kuimarisha uelewa wa wakulima na wadau kuhusu fursa zilizopo katika tasnia ya mbolea, hususan kwa vijana na wanawake, kwa lengo la kuchochea ubunifu, kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kilimo na kuendeleza kilimo endelevu nchini.

Post a Comment

0 Comments

PPRA YANG'ARA KILELE MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026