Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Joseph Mafuru akipanda mti katika Kata ya Chang'ombe.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
MKURUGENZI Wa jiji la Dodoma Joseph Mafuru amesema kuwa wameanza zoezi la usafi kata kwa kata lengo likiwa ni kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi ambapo leo alishiriki kufanya usfi na kupanda miti katika Kata ya Chang'ombe.
Akizungumza mara baada ya kufanya usafi leo Februari 5, 2022, jijini hapa amesema wanafanya vitu viwili kwa wakati mmoja ambavyo ni usafi wa mazingira na kupanda miti.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa wameshatembea katika kata sita za jiji la Dodoma na kwamba wanaendelea kuhamasisha jamii kufanya usafi.
"Sheria za mazingira zipo na wananchi wengi hawazifahamu kwa wale wanaozifahamu wamekuwa hawazizingatii lakini sheria zipo na zinabana faini kubwa kwani ni kuanzia 50,000 hadi 300,000," ameongeza.
Hapa tumewasikia wananchi wa kata hii ya Chang'ombe mtu anatoka nyumbani kwake anakuja kutupa mfuko wa Pampas katika eneo la shule sasa tunafanya vitu viwili tunatoa elimu," amesema.
Mafuru amesema wanatekeleza sheria ya mazingira na ndio maana wanaongozana na polisi jamii pale watakapo mkuta mtu anachafua mazingira hapo hapo anachukuliwa hatua.
Mbali na hilo mkurugenzi huyo amefafanua kuwa wamesambaza miti kwenye shule zote Milioni 1.5 kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira amesema Seleman Jafo anavyohamasisha watoto kusimamia miti yao.
Kwa upande wake,Afisa Mazingira wa Jiji la Dodoma,Dickson Kimaro amesema wamekuwa wakiendelea na zoezi la utoaji wa elimu kuhusu uzoaji taka ambapo kaya nyingi zimekuwa zikujitokeza kufanya usafi.
0 Comments