CAG:KUNA ONGEZEKO LA TRILIONI 7.76 DENI LA SERIKALI


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani),wakati akiwasilisha ripoti yake kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2020/ 2021.

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za  Serikali (CAG), Charles Kichere amesema  matokeo ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu umebaini kuwa mwenendo wa deni la serikali hadi kufikia Juni 30 mwaka 2021 lilikuwa shilingi trilioni 64.52 ikilinganishwa na trilioni 56.76 mwaka 2019/ 2020.

Hayo yamesemwa leo Aprili 12 2022 jijini hapa na CAG, Kichere wakati akiwasilisha ripoti yake kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2020/2021 amesema kuwa kuna ongezeko la shilingi  trilioni  7.76 sawa na asilimia 13.7 ikilinganishwa na ongezeko la trilioni 3.65 sawa na asilimia 7 mwaka uliopita.

CAG amefafanua kuwa kipimo cha deni hilo la serikali kinachotumia pato la Taifa kinaonesha kuwa deni ni himilivu na kwamba usimamizi wa mapato yatokanayo na kodi katika mwaka wa fedha 2020/2021 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilikusanya shilingi trilioni 17.59 kwa Tanzania Bara ikilinganishwa na makisio ya shilingi trilioni 20. 29.

Ameongeza kuwa makusanyo hayo ni pungufu kwa kiasi cha shilingi trilioni 2.70  sawa na asilimia 13.3 ya makisio hayo.

 "TRA ilikusanya shilingi bilioni 299. 08,kwa upande wa Zanzibar ukilinganisha na makisio ya shilingi bilioni 383.54, makusanyo haya ni pungufu kwa kiasi cha shilingi bilioni 84.46 sawa na asilimia 22 ya makisio," amesema CAG Kichere.

Amefafanua kuwa TRA ilikuwa na changamoto katika ukusanyaji mapato ikiwamo mafuta kuingia nchini bila kuainishwa kama ni kwajili ya matumizi ya ndani  au kusafirishwa nchi jirani  yenye ushuru wa forodha  shilingi bilioni 2.89.

" Nilibaini miamala 17 yenye jumla ya lita milioni 31.12 za mafuta yenye makadirio ya ushuru wa forodha shilingi bilioni 2.89 ambayo haya kuainishwa kama ni kwa matumizi ya ndani au ya kusafirishwa kwenda nchi jirani," amesema.

Amesema kuwa hiyo inaashiria kwamba mafuta hayo yalitumika nchini na yalipaswa kutozwa ushuru  wa forodha shilingi bilioni 2.89.

" Ninapendekeza serikali iimarishe mifumo ya udhibiti na usimamizi wa mafuta yanayoingia nchini ili kuzuia matumizi ya mafuta haya nchini bila kodi stahiki kulipwa," ameeleza CAG.



Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU