Mwenyekiti wa chama wa chama Cha Mafundi Tanzania (TASMEA),Mpasi Kiera akizungumza na waandishi wa habari.
Katibu wa chama Chama Cha Mafundi Tanzania (TASMEA), Alewangwa Muro akisoma risala ya chama hicho.
Mhadhiri Mwandamizi na Kaimu Mkurugenzi wa chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE), Kampusi ya Dodoma, Dk. Robert Mashenene alifafanua jambo kwa viongozi na Wajumbe wa Chama Cha Mafundi Tanzania (TASMEA),
Baadhi ya wajumbe wa chama Cha mafundi Tanzania(TASMEA),waliohudhuria mkutano.
Na Asha Mwakyonde,Dodoma
MAFUNDI Mizani Tanzania wametakiwa kujiendeleza kiufundi ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia kwani vipimo vya kimekanika vitaisha masokoni na badala yake vipimo vya kidigitali vinahitaji uelewa wa masuala ya kielektroni.
Pia takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa kuna mafundi mizani wenye leseni 274, na asilimia 40 wapo mkoa wa Dar es Salaam hivyo wameshauriwa kufungua ofisi mikoani kwani wananchi wanahitaji huduma ya vipimo katika mikoa ambayo haina fundi hata mmoja.
Hayo yamesemwa leo jijini hapa Aprili 11, 2022 na Meneja Sehemu ya Ukaguzi na Ufuatiliaji ( Surveillance),Makao Makuu Wakala wa Vipimo, Almachius Pastory wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa viongozi na kujadili changamoto za Chama Cha Mafundi wa Mizani Tanzania (TASMEA),wa siku mbili amesema mafundi hao bila kujiendeleza kazi zao zitafanywa na wageni.
Amesema kuwa kipimo ni nyenzo muhimu katika kubadilishana bidhaa na fedha hivyo ili biashara ifanyike kwa haki lazima vipimo sahihi vitumike na muundaji wa vipimo hivyo lazima aunde chenye usahihi.
"Marekebishaji wa vipimo lazima ahakikishe vipimo vyote alivyorekebisha vinakidhi matakwa ya sheria ya vipimo sura 340.Mfano kipimo kisichokidhi matakwa ya sheria ya vipimo kinaweza kuzidisha au kupunguza uzito wa bidhaa," amesema.
Meneja huyo amefafanua kuwa kuzidisha kipimo kunampa hasara mwenye mali, duka na mfanyabiashara kumfanya asipige hatua katika biashara yake, na kwamba kupunguza kunasababisha mnunuzi kupata bidhaa pungufu ya pesa aliyotoa.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Mpasi Kiera amesema kuwa mkutano huo una mambo matatu, kufanya uchaguzi wa viongozi, kufahamiana na mafundi kutoka mikoa mbalimbali ya nchi na kujadili taalamu yao ili kuendana na sayansi na Teknolojia ya sasa.
Mwenyekiti huyo Kiera ameeleza kuwa kupitia chama wataweza kushirikiana na kuhamasishana ili waweze kufikia wanapo pahitaji pamoja na kuendana na ulimwengu wa sasa wa kidigitali.
Ameongeza kuwa kwa sasa kuna mizani za kisasa bila ya kushirikiana na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), hawawezi kupata mafunzo ya kutosha ya kujiinua katika taaluma yao ya ufundi wa mizani.
" Tunakishukuru chuo cha CBE kwani mafundi wengi wamepata mafunzo ya yanayoendana na mizani za kidigitali," amesema Mwenyekiti huyo Kiera.
Awali akisoma risala Katibu wa chama hicho Alewangwa Muro amesema kuwa dira ya chama Cha mafundi Tanzania ni kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa mafundi hao ili kukabiliana na maendeleo ya sayansi na Teknolojia kwa wakati uliopo.
"Katika hili tumepata mafanikio kwa kushirikiana na Chuo cha CBE kwa kutupatia mafunzo ya muda mfupi. Hivyo tunaendelea kushirikiana na chuo kiweze kutupatia mafunzo zaidi," ameeleza Muro.
Pia ameeleza kuwa dira yao nyingine ni kujiunga na vyama vya mafundi mizani Afrika Mashariki,Afrika na Duniani kwa ujumla na kushirikiana navyo ili kuboresha taaluma na kupanua wigo, maarifa kwa viwango vya juu.
Aidha amefafanua kuwa chama hicho kilianzishwa mwaka 2014 kama wazo la kikundi cha watu 53 waliokutana na kuamua kuanzisha umoja ili waweze kuwa msaada kwa mafundi mizani kwa kuboresha taaluma ya ufundi na pia iwe rahisi kusaidiana wakati wa changamoto mbalimbali za kiufundi.
Naye Mhadhiri Mwandamizi na Kaimu Mkurugenzi wa chuo Cha CBE, Kampusi ya Dodoma, Dk. Robert Mashenene, amesema chuo hicho kimekamilisha ujenzi wa maabara katika kampasi hiyo na kwamba mwezi ujayo wataanza kutangaza udahili wa wanafunzi.
"Hii ni Habari njema. Tunawashukuru sana wakala wa vipimo walitutia moyo wakati tunaanza program hii na wametuahidi kutupatia wataalamu wa kutoa mafunzo," amesema Mhadhiri huyo.
Dk.Mashenene amewataka mafundi hao pale wanapohitaji mafunzo ya muda mfupi wanakaribishwa kwani kampasi hiyo ni ya Umma watapatiwa ushirikiano.
0 Comments