Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na watoto wakati maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika jijini Dodoma tarehe 16 Juni, 2022.
Watoto kutoka shule mbalimbali za Manispaa ya Dodoma wakiingia katika viwanja vya Nyerere Square jijini hapo kwa maandamano rasmi kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kimkoa, ambapo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameshiriki maadhimisho hayo tarehe 16 Juni, 2022. Mwenyekiti wa Kampeni ya SMAUJATA Sospeter Bulugu akimpatia fulana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ikiwa ni uzinduzi wa kampeni hiyo na maadhimisho ya Siku ya mtoto wa Afrika jijini Dodoma tarehe 16 Juni, 2022.
Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Malaamu Dk Dorothy Gwajima amewataka wanaume kusimama na kupinga vitendo vya ukatili vya kulawitiwa na kubakwa watoto vinavyofanywa na baadhi ya wanaume hao huku akimtangaza mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Hamisi Shaban kwa jina maarufu Babu Tale kuwa balozi wa kupinga ukatili kwa watoto hao.
Pia Waziri huyo amezindua kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha wananchi wote kuungana kupinga vitendo vya ukatili wa aina zote kwenye jamii ijulikanayo Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA), imezinduliwa rasmi katika kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika mkoani Dodoma.
Dk. Gwajima ameyasema hayo jijini Dodoma Juni 16, 2022 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika Duniani yalifanyika katika viwanja vya Nyerere Skwea yenye kauli mbinu isemayo “Tuimarishe ulinzi wa Mtoto; Tokomeza Ukatili Dhidi Yake: Jiandae kuhesabiwa.
Waziri Gwajima amesema kuwa anashangazwa na wanaume kwani hawajawahi kujitokeza kupinga vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto hao huku wakikaa kimya bila kuzungumzia suala hilo
Ameaema kauli mbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kuwalinda Watoto dhidi ya ukatili na hatimaye kuvitokomeza kabisa huku akiwahimiza wananchi wote kujiandaa na kujitokeza kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi tarehe 23 Agosti, 2022.
Ushiriki wa wananchi kwenye sensa hii utaiwezesha Serikali kupata taarifa na takwimu kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya Taifa.
Ameongeza kuwa msingi mkuu wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni utoaji wa Haki za Mtoto kama ilivyoelekezwa na Umoja wa Afrika katika Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1991 na kwamba Umoja wa Afrika umetohoa maazimio hayo kutoka katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989.
Dk. Gwajima amefafanua katika kuimarisha utekelezaji wa haki, ulinzi na ustawi wa mtoto nchini, Serikali imeendelea kufanya mambo mbalimbali;
Iliandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ambayo imeainisha Haki tano (5) za Msingi za Mtoto ambazo ni Haki ya Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na haki ya Kutobaguliwa.
"Wizara imeratibu utungwaji wa Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 na sasa inafanyiwa mapitio katika baadhi ya vipengele pamoja na kanuni zake ili ziweze kukidhi mahitaji ya sasa katika utoaji wa haki kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa mtoto nchini," amesema.
Amesema serikali imefanya marekebisho kwenye baadhi ya vifungu vya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kwa kuongeza kipengele kinachotoa adhabu ya kifungo cha hadi miaka 30 kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi au kuhusika katika kukatisha masomo yake kwa kumuozesha ama kumuoa.
Pia Dk. Gwajima amesema serikali imeweza kuongeza idadi ya Mahakama za kusikiliza mashauri ya watoto kutoka mahakama 3 kwa mwaka 2015/2016 hadi kufikia Mahakama 141 Januari 2022.
Kwa upande wake Babu Tale amesema amejitolea kuwa balozi wa kupinga ukatili, kusimama na kuhamasisha wanaume wenzake kupinga ukatili huo unaofanywa na baadhi ya wanaume wenzao.
"Nina watoto wa kiume na wakike najua ugumu wa malezi ya watoto hivyo nasimama kupinga ukatili huu na nitaenda kuwahamasisha wanaume wenzangu bungeni tuungane pamoja kupinga ukatili," amesema Babu Tale.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma a Maendeleo ya Jamii Stanslaus Nyongo amesema kuwa wapo bega kwa bega na Dk. Gwajima katika kuhakikisha ukatili huo unatokomezwa.
Amesema kuwa wameshuhudia utekelezwaji wa uanzishwaji madawati ya kijinsia pamoja na kuanzishwa huduma jumuishi kwa ajili ya kupinga masuala ya vitendo hivyo.
0 Comments