Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),Dk. Fatma Khalfan kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mohamed Khamis Hamad wakati akisoma tamko la tume hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya ualbino..
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WANANCHI wametakiwa kutoa taarifa katika mamlaka husika juu ya vitendo vya kikatili, udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya Watu Wenye Ualbino katika maeneo yao pia waachane na imani, mila, desturi na mitazamo potofu ambayo huwafanya Watu hao kujiona hawakubaliki, hawawezi na hawana mchango kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma jana na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),Dk. Fatma Khalfan kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mohamed Khamis Hamad wakati akisoma tamko la tume hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa kuhusu Ualbino amesema wataaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za Watu Wenye Ualbino zinalindwa, zinakuzwa na kutetewa nchini.
Ameongeza kuwa Tume hiyo inaungana na wadau wa utetezi wa haki za Watu Wenye Ualbino duniani kote katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa Kuhusu Ualbino.
"Siku hii ni ya kipekee kwetu sote kwa kuwa inatukumbusha umuhimu kwa Serikali, Asasi za Kiraia, taasisi za dini na wadau wengine kutoa elimu kwa umma kuhusu ualbino na haki za Watu Wenye Ualbino,". ameaema.
Ameeleza kuwa Kauli mbiu ya mwaka huu ni:“Kuelekea sensa ya watu na makazi, tuimarishe upatikanaji wa takwimu bora kwa maisha bora. Watu Wenye Ualbino tujitokeze kuhesabiwa.”
Ameongeza kuwa kauli mbiu hiyo ni muhimu kwa sababu takwimu sahihi ya watu na makazi itawezesha Serikali kupanga mipango yake kwa usahihi na kufikia malengo ya kitaifa pamoja na kutambua makundi mbalimbali, ikiwemo Watu Wenye Ualbino.
Kamishna huyo amefafanua kuwa kauli mbiu hiyo pia inaenda sambamba na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu inayoelekeza uwepo wa kanzi data ya watu wenye ulemavu.
Amesema THBUB inatambua jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wadau mbalimbali wa haki za binadamu katika kuongeza uelewa kuhusu ualbino na haki za Watu Wenye Ualbino.
"Pamoja na jitihada hizi THBUB imebaini uwepo wa vitendo ambavyo ni kinyume na haki za binadamu na utu wa mtu dhidi ya Watu Wenye Ualbino.Vitendo hivi vinapaswa kupingwa na kulaaniwa na kila mmoja wetu," amesema Dk. Khalfan.
Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya utetezi wa haki za binadamu kuendelea kutoa elimu kuhusu ualbino na haki za watu wenye ualbino.
Dk. khalfan ameomba zoezi la Sensa ya watu na makazi, Serikali iwatambue Watu Wenye Ualbino na kuweka mikakati endelevu ya kuendelea kuwatambua kwenye maeneo yao.
Pia amesema serikali za mitaa na vijiji zifuatilie ili kubaini vitendo vya uvunjifu wa haki za Watu Wenye Ualbino katika maeneo yao na Jeshi la Polisi nchini lihakikishe watuhumiwa wa vitendo vya ukatili dhidi ya Watu Wenye Ualbino wanapatikana na kufikishwa mahakamani.
0 Comments