VIONGOZI WA MIKOA WATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO KWA WAJANE




Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Malaamu Dk Dorothy Gwajima.

Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Malaamu,Dk. Dorothy Gwajima amewataka viongozi wa mikoa yote kuimarisha ushirikiano na wajane kupitia vyama vyao ili kutambua mahitaji ya wajane katika maeneo yao na kutafakari hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kutoa majawabu ya upatikanaji wa mahitaji yao katika familia.

Pia amewaomba viongozi wa vyama vya wajane kuripoti kwenye ofisi za serikali ili wajitambulishe wafahamike kwa ajili ya kupata ushirikiano imara zaidi. 

Dk.Gwajima ameyasema hayo Juni 22, 202,jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yenye kaulimbiu inayosema "Utu Uwezeshaji wa Kiuchumi na Haki za Kijamii kwa Wajane amnayo imetokana na Kaulimbiu ya Kimataifa inayosema Dignity  Economic Empowerment and Social Justice for Widows" amesema kaulimbiu hiyo  inahimiza jamii kuhakikisha kuwa inawathamini wajane kwa kuwapatia haki zao na kuwawezesha kiuchumi. 

Waziri huyo pia anetumia nafasi hiyo kuwakumbusha wajane na wanahabari kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa Agosti  23, mwaka huu kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. 

"Sisi wanawake ni kundi ambalo tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kuitikia zoezi la sensa huku tukielimisha wengine, " ameaema Dk. Gwajima.

Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inakadiria kuwa idadi ya wajane nchini Tanzania ni laki 8.8 ambayo ni sawa na asilimia 3.1 ya wanawake wote nchini ambao wanakadiriwa kuwa millioni 28.5 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019.  

Dk. Gwajima ameeleza kuwa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inawatambua na kuwaenzi  wanawake wote pamoja na makundi maalum wakiwemo wajane. 

Amesema juhudi mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na Serikali  yake ili kuhakikisha  changamoto zinazowakabili wajane zinatatuliwa. Juhudi hizo ni pamoja na kuitambua Siku ya Wajane Duniani sambamba na kushirikiana na wadau kuweka mikakati ya kutatua changamoto za wajane kama ilivyobainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

 Waziri huyo ameongeza kuwa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000, na mpango wa Mkakati wake wa mwaka 2005, Maazimio ya ulingo wa Beijing, Ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na Ajenda ya Maendeleo ya Bara la Afrika  2063.

" Naomba kutumia  fursa hii kuwasihi waandishi wa habari na wadau wote kuungana na Serikali katika kufichua ukiukwaji wa haki kwa wajane ili waweze kupatiwa msaada wa kisheria pale inapohitajika, pia kuongeza juhudi zaidi katika kukabiliana na vitendo vya ukatili, unyanyasaji na kuwainua wajane ili wapate uwezo wa kiuchumi wa kuzihudumia familia zao zilizoachwa na wenza wao," amesema.

Inakadiriwa kuwa idadi ya wajane Duniani ni takriban millioni 258 na kati ya hao, wajane 115 millioni wanadhulumiwa, wanafanyiwa ukatili, wanakabiliwa na umaskini na kutengwa na jamii; na mjane mmoja (1) kati ya kumi (10) anaishi katika umasikini uliokithiri. 



Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI