CCM YARIDHIA UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA


Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa Itikadi na Uenezi (NEC), Shaka Hamdu Shaka.

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

KATIBU wa Halmashauri Kuu Taifa Itikadi na Uenezi (NEC), Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa Chama Cha Mapindizi (CCM) kupitia kikao cha Halmashauri hiyo  kwa kauli moja kimekubaliana upatikanaji wa Katiba Mpya na kimeona umuhimu wa katiba  hiyo kwa kuzingatia mazingira ya sasa.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kimefanyika katika ukumbi wa White House Makao Makuu ya Chama Jijini hapa chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho Samia Suluhu Hassan.

Katibu huyo ameyasema hayo Juni 22,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa  kuhusu yaliyojiri katika vikao vya kamati kuu na Halmashauri kuu ya Taifa ya Chama hicho amesema pia CCM kinaishauri serikali kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa katiba mpya.

Shaka Hamdu Shaka ameongeza kuwa lengo la katiba hiyo mpya kwa maslahi mapana ya Taifa na Maendeleo ya Watanzania wote.

"Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Husein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuonesha uvumilivu na ukomavu wa kiuongozi katika kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa hali inayochochea umoja, amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo kuharakisha maendeleo yao," amesema.

Ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefanya uteuzi wa wenyeviti wa halmashauri za wilaya na Mameya ambapo kimewateua Erasto Mpete kuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Mji na Mohamed Bayo kuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Shaka Hamdu Shaka amesema pamoja na mambo mengine Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza  Rais Samia Suluhu Hassan kwa ukomavu, ustahimilivu, uhodari na dhamira yake njema ya kufanya maridhiano na vyama vya siasa nchini kwa lengo la kuimarisha umoja, ushirikiano, mshikamano, amani na utulivu kwa maendeleo na ustawi wa watanzania wote.

Halmashauri kuu ya Taifa imevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kukubali kuunga mkono hatua hiyo. Chama kimeishauri serikali kuharakisha utekelezaji wa masuala yote yatakayojenga kuaminiana, kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa kwa ustawi wa wananchi wote,' amesema. 

Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo ambayo Halmashauri Kuu imeshauri kutazamwa ni pamoja na kesi zenye sura ya kisiasa kwa wafuasi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa nchini.

Katibu huyo ameeleza chama kimeishauri serikali utekelezaji wa masuala yote ya kuimarisha demokrasia nchini na mazingira ya kisiasa yafanyike bila kuathiri uhuru na usalama wa nchi yetu.

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama hicho amesema halmashauri Kuu ya Taifa imepokea na kuridhishwa taarifa ya maendeleo ya uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama ambao umeshakamilika kwa asilimia 99.5 katika ngazi ya mashina na matawi kote nchini na sasa upo katika ngazi ya Kata au Wadi.

Amesema Chama kimetakiwa kuzifanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika ngazi hizi ili kuimarisha ushiriki wa haki, usawa na demokrasia katika ngazi zote zinazofuata kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi ya Chama. 

Pia ameongeza kuwa halmashauri Kuu ya Taifa imefanya uchaguzi wa kujaza nafasi mbili za wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa zilizokuwa wazi kwa kuwachagua kwa kura  Stephen Masatu Wassira na Theresia Adriano Mtewele.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI