MFAHAMU MWANAMKE ALIYEANZA BIASHARA YA KUTEMBEZA VITAMBAA HADI KUMILIKI HOTELI


 Mkurugenzi Mkuu wa Hoteli ya Four Point and Hall Kitolina Kippa.

Muonekano wa Hoteli ya Four Point and Hall

Na Asha Mwakyonde, Dodooma

‘’NILIANZA kuuza vitambaa vya magauni ya wanawake nilikuwa nikiwaambia wanaume mpende mkeo naye atakupenda mnunulie uone atakavyokupenda na nilikuwa nauza kweli nikiwaambia hivyo, haya ni maeneo ya Mkurugenzi Mkuu wa Hoteli ya Four Point and Hall Kitolina Kippa.

Akizungumzia historia ya namna alivyoanza biashara hadi kufanikiwa kuwa mmiliki wa hoteli ya Four Poini iliyopo jijini Dodoma barabara ya Morogoro amesema ndoto yake kubwa ilikuwa ni kumiliki biashara kubwa.

Kitolina amesema mwaka 2012 alifanikiwa kuanzisha biashara ya ndoto yake  na kwamba kabla ya kuwa mkurugenzi alikuwa mtumishi wa Umma aliyeajiriwa kama afisa mtumishi ambapo aliendelea kuwa mtumishi hadi kuwa mkurugenzi wa rasilimali watu katika utumishi wake serikalini.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa aliajiriwa ofisi ya Bunge la Tanzania ambapo amefanya kazi miaka 26 hadi mwaka 2016 ndipo alipohama ofisi hiyo na kwenda Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Akiwa katika Ofisi ya Bunge Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa aliwahikufanya kazi na Maspika watano wa Bunge hilo ambao ni Adamu Mkwawa, Pius Msekwa, Samweli Sitta na Anne Makinda  na wakati anatoka katika Ofisi hiyo Job Ndugai   anaingia  mwaka 2015.

Ameeleza kuwa pamoja na kuwa mtumishi alikuwa akijishughulisha na biashara ndogo ndogo ya kuuza vitambaa vya magauni ya wanawake.

‘’Nilikuwa nikisafiri kwenda Zanzibar wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri usiku, nilikuwa naondoka siku ya Ijumaa naenda kulala Dar es Salaam Jumamosi naenda Zanzibar na kugeuza nalala tena Dar es Salaam siku ya Jumapili narudi Dodoma sijawahi kutumia muda wa siku za kazi hata siku moja,”amesema.

Mkurugenzi huyo Kitolina amefafanua kuwa biashara hiyo ya vitambaa ilikuwa ya mkononi alivitembeza kutafuta soko ambalo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupata wateja huku akisema pia ameuza mashati juliyokuwa yakijulikana kama mashati ya Mandela ambayo aliwauzia wabunge.

Amefafanua kuwa baada ya kuona mtaji wake umeanza kukua akafungua duka la kuuza nguo ambapo alikuwa akienda Dar es Salaam kununua kwa bei ya jumla katika soko kuu la Kariakoo huku akieleza kwamba biashara hiyo ameifanya kwa muda wa miaka nane.

Pamoja na posho aliyokuwa akiipata katika utumishi wake wa Umma na ile faida  alikuwa akiweka akiba mkurugenzi huyo amesema  alifikiria kufanya biashara ya kudumu na ambayo ilikuwa ni ndoto yake.

“Ndoto yangu ya siku nyingi ilikuwa kumikili hoteli kubwa na ya kisasa ambayo tayari nimeshaitimiza ndoto yangu namshukuru Mungu, lakini wakati nafanya biashara nilikuwa na mume wangu baadae akafariki na kubaki mjane tangu  mwaka 2000,”ameeleza.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa  mume wake alifariki akamuacha katika hali mbaya kwa kuwa alikuwa na siku tatu tangu amefanyiwa upasuaji wa mtoto huku akisema  alikuwa na majonzi pamoja na maumivu.

Katolina amebainisha kuwa hakuweza kukata tamaa ya kujishughulisha kwani mume wake alimuachia watoto watatu wakiume wawili na wakike mmoja na kwamba hakutegemea msaada kutoka kwa wanafamilia, ndugu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo “Nikaona sasa ndio wakati wa kujishughulisha zaidi niliendelea kufanya zile biashara pamoja na duka nililokuwa nalo lakini baadhi ya bidhaa nikawa naenda kutembeza mkononi katika mitaa mbalimbali pamoja na kuwauzia wafanyakazi, ’’.

Amesema kuwa baadae akafikiria kuomba mkopo wa mshahara wa watumishi ambapo alikopo benki ya CRDB huku akiishukuru benki hiyo kwa kumwamini na kumkopesha kwa mara ya kwanza milioni 50.

UJENZI WA HOTELI

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa baada ya kupata fedha hizo kuzichanganya na zile za faida ya biashara na kwa kuwa tayari alishanunua kiwanza alianza ujenzi wa hoteli hiyo  ili kutimiza lengo lake.

“Nilianza ujenzi wa hoteli hii huku narejesha ule mkopo wakati nakaribia kumaliza benki ya CRDB wakaniongezea tena milioni 50 nyingine hapo nikawa nimepata uwezo wa kuendelea na ujenzi hatimaye nikamiliza,”amesema Mkurugenzi huyo.

Ameeleza kuwa baada ya kumaliza ujenzi huo aliishiwa na fedha ambapo alikaa kukusanya nguvu ili aweze kununua vitu vya samani za ndani lakini baadae alikutana na meneja wa benki ya NMB ambapo alimshauri asikae kwani ujenzi wa hoteli ulishakamilika atapoteza fedha hivyo  benki hiyo ikamkopesha milioni 50 ili kukunua samani za ndani.

Pia Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa alikopo benki ya Micro finance milioni 25 ambapo alianza kurejesha kidogo kidogo kote alipokopa huku akieleza kwamba anamshukuru Mungu pamoja na mikopo yote hiyo aliweza kuwasomesha watoto wake katika shule nzuri za binafisi.

CHANGAMOTO

Akizungumzia changamoto alizokutana nazo wakati akianza ujenzi wa hoteli amesema kuwa ni nyingi kutokana na baadhi ya watu kumkatisha tamaa kwamba ni mwanamke hawezi kufika mbali katika ujenzi huo.

“Changamoto ni nyingi kuna wakati mwingine baadhi ya watu wananikatisha tamaa na unaweza kukubaliana na mawazo yao kwa kuwa unafika mahali umeishiwa na fedha unaanza kuyakumbuka yale waliyokuwa wakiyasema,”ameongeza.

Lakini sio wote wanaokukatisha tamaa nilikutana na baadhi ya watu akiwamo mkurugenzi mmoja anayemiliki hoteli kubwa hapa Dodoma alinipa moyo wa kuendeleza,”amesema.

WITO WAKE KWA WANAWAKE

Mkurugenzi huyo amewataka wanawake kutokukatishwa tamaa na badala yake wakisimamie kile wanancho kiamini watafika mbali kimaendeleo.

“Nawashauri wanawake wenzangu kama mtu anapika maandazi, vitumbua, anauza juisi au anapika mama lishe asimamie vema biashara yake itamfikisha mbali katika malengo yake. Wapo wanafanya bashara hizo na kujidharau kwa kuona haina maana,”amesema.

Ameongeza kuwa biashara yoyote pasipokuwa na malengo mtu hawezi kufanikiwa jambo la kwanza ni kuwekeza nguvu, akili na maarifa yote katika biashara ambayo mtu huyo anaifanya.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa wanawake wamekuwa ni wahanga wakubwa wa kukatishwa tamaa wanapofanya miradi mikubwa ya kimaendeleo kwa kuonekana hawana uwezo wa kufanya, kusimamia jambo kubwa kama ilivyo kwa wanaume.

" Sisi Wanawake tunatakiwa tusimame mawazo yetu kitu cha msingi tujitambue, jitambue wewe ni wewe hakuna mtu atakayekuja kusimama kwa niaba yako, mimi ni Kitolina Kippa nitabaki kuwa Kitolina Kippa hakuna atakayekuja kusimama kwa niaba yangu," amesema.

Kitolina amewasisitiza kuwa baada ya kujitambau wanawake hao waamini wanachokifanya kwa kuwa anachokifanya mwanaume na wao wanaweza.

Kwa mujibu wa Kitolina hata matajiri wanaoonekana wengine walianza kuuza Karanga, kushona viatu hivyo unaanza na kitu kidogo huku ukiweka akiba faida unayoipata  pamoja na kuwa na mipango ya baadae.

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Machi 8 ni siku ya Wanawake Duniani,mwaka huu Kitolina amepata tuzo ya mwanamke mwenye uthubutu na
mwenye mafanikio ambayo alikabidhiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi,8 kila mwaka ilianza kuadhimishwa 1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuridhia siku hiyo kutumika kama siku rasmi ya kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake.

Siku hii pia huongeza chachu katika harakati za mapambano katika usawa wa kijinsia kwa wanawake na wanaume katika jamii.

Post a Comment

0 Comments

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA