NA ASHA MWAKYONDE,DODOOMA
SERIKALI imetoa shilingi bilioni 111.8 kwa ajili ya miradi 12 kati ya miradi hiyo minne ni mipya, mitano ya kukarabati na mitatu ni ile inayoendelea.
Akizungumza jijini hapa November 1,2022 Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Eric Hamissi
wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo amesema Kati ya bilioni 53.9 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi 7 ya ziwa Tanganyika .
Mkurugenzi huyo Amefafanua kampuni hiyo inatekeleza miradi Mitatu ya ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo ya MV Mwanza na mradi wa ukarabati wa meli ya Mizigo ya MV Umoja zote za Ziwa Victoria mradi wa ukarabati wa meli ya kubeba mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika.
Ameongeza kuwa mkataba wa ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza itakayobeba abiria 1,200 na mizigo tani 400 katika Ziwa Victoria ulisainiwa Septemba 03, 2018 na utekelezaji wake ulianza Januari 17, 2019. Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani 46,926,251.40 sawa na Shilingi bilioni 108.5 za Kitanzania.
“Hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa jumla ya fedha za Kitanzania Shilingi bilioni 76.35 sawa na asimilia 72 ya gharama na mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2023 kulingana na mkataba na mradi umefikia asilimia 73 ya utekelezaji”amesema.
Ameeleza kuwa Mkandarasi ameendelea kuagiza vifaa mbalimbali vya kumalizia umbo la meli (finishing) na kwa sasa vifaa vilivyobaki ni vya malazi (accommodation), viti na vifaa vingine vya uendeshaji wa meli (navigation), vifaa vya umeme pamoja na kupaka rangi awamu ya mwisho.
Aidha akizungumzia mkataba wa ukarabati wa meli ya MV Umoja yenye uwezo wa kubeba tani 1200 za mizigo katika Ziwa Victoria alisema kuwa ulisainiwa Juni 15, 2021 na utekelezaji wake ulianza Novemba 25, 2021.
“Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani 8,422,840 sawa shilingi 19,811,446,192.40 za Kitanzania ambapo Mkandarasi ameshalipwa malipo ya awali ambayo ni asilimia 15 sawa na fedha za Kitanzania 2,971,716,928.80 na kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 4”amesema.
Lakini pia mkataba wa mradi wa ukarabati wa meli ya MT. Sangara yenye uwezo wa kubeba tani 350 sawa na lita 410,000 za mafuta wake ulisainiwa Mei 26, 2021 na unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani 3,606,595.00 sawa na Shilingi 8,349,267,425.
Amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa muda wa miezi 12 kwa gharama ya Dola za Kimarekani 3,606,595 sawa Shilingi 8,349,267,425. Utekelezaji wa mradi huu ulianza Novemba 8, 2021 na unatarajiwa kukamilika Novemba 7, 2022.
“Mpaka sasa Mkandarasi ameshalipwa malipo ya awali ambayo ni asilimia 15 sawa na fedha za Kitanzania 1,252,390,113.75 na kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 72," amesema.
Akizungumzia vipaumbele vya MSCL amesema kuwa ni pamoja na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati kuendana na thamani ya fedha iliyotengwa na kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi wa Tanzania na nchi za Jirani.
Pia ameongeza kuwa kampuni hiyo inafanya utafiti wa kimasoko katika mikoa iliyopo kwenye mwambao wa maziwa yetu makuu na nchi za jirani hasa Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Uganda.
"Nchi hizi hazina milango ya bahari na hivyo ni fursa kubwa kwa Kampuni na nchi kwa jumla kurahisisha uvushaji wa mizigo inayokwenda kwenye nchi hizi kwa wingi na kwa muda mfupi," amesema.
Aidha ameeleza kuwa wanafahamu kuna usindani katika usafiri wa kutumia barabara lakini ni ukweli usiopingika kuwa usafiri wa njia ya maji ni rahisi, nafuu na wa haraka kuliko kutumia barabara katika kuzifikia nchi hizo za jirani lengo likiwa ni kuongeza pato la nchi kwa kusaidia kusafirisha bidhaa nyingi zaidi kwenda nchi zisizokuwa na milango ya bahari kwa kutumia meli zilizopo kwenye maziwa makuu.
0 Comments