DUNIA YA SASA INAHITAJI WATAALAMU WA USTAWI WA JAMII-WAZIRI GWAJIMA


 Na WMJJWM, Mwanga, Kilimanjaro

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Dunia ya sasa inawahitaji wataalamu wa Ustawi wa Jamii Ili kusaidia kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizoibuka sambamba na maendeleo ya Dunia.

Akizungumza katika mahafali ya 5 ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Kampasi ya Kisangara, Mwanga, Kilimanjaro Desemba 15, 2022, Waziri Dkt. Gwajima amesema Wahitimu hao wana fursa ya kutatua changamoto za kijamii hasa za kisaikolojia zinazowakumba watu wengi. Aidha, pamoja na changamoto ya ajira iliyopo, ni vema Wahitimu hawa wakati wakisubiri ajira wawe na maono ya kugeuza changamoto za kijamii kuwa fursa.

"Nimegundua, taaluma hii ya ustawi wa jamii ni kubwa na inayohitaji wenye moyo wa maadili na upendo kwa sababu inalenga kuwasikiliza wakiwemo wanaolia machozi na kukosa tumaini, hivyo wanataaluma hawa wanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la pekee hasa kwenye zama hizi ambapo maendeleo yameleta pia machozi mengi" amesema Waziri Gwajima.

Waziri Dkt  Gwajima ameendelea kusema kwamba, msingi mkuu wa wasomi kuelimika ni kuwa na uzalendo kwa nchi yao hivyo ni matumaini yake wahitimu hao watafanya vizuri kwa kusimamia misingi na maadili ya taaluma.

Ameongeza kwamba, Wizara imeweka miongozo na kanuni kuhusu suala la malezi ya watoto kuanzia ngazi ya familia na vituo vya kulelea watoto na kuipongeza kwa mara nyingine taasisi hiyo kwa kuunda mitaala ya malezi na makuzi.

"Namuagiza Kamishna wa Ustawi wa Jamii kukaa na Menejimenti ya taasisi kuona namna gani inaweza kuanza kutoa vyeti katika eneo la malezi na makuzi na saikolojia ili kuimarisha ustawi" ameongeza Waziri Gwajima.

Dkt. Gwajima hakusita kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Wizara hiyo kwa lengo la kuhakikisha ustawi wa watanzania unaimarika na kusisitiza ushirikiano wa wadau wote.

Halikadhalika, ameipongeza taasisi kwa kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine kama SOS Children Villages, Investing Children and their Society (ICS) pamoja na Karibu Tanzania Organisation (KTO) katika kupanua wigo wa mafunzo na huduma hasa kwenye nyanja ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto, kuhakikisha mtoto analindwa dhidi ya aina zote za ukatili, ambayo ni hatua kubwa katika kuimarisha uwezo wa taasisi kutoa huduma.

Wakati huo huo Waziri Dkt. Gwajima zindua rasmi madarasa mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 370 na ofisi mbili yaliyojengwa kwa fedha za ndani kwa kutumia wataalamu wa chuo cha Maendeleo ya Jamii na Ufundi Mabughai. 

Aidha, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa bweni la wanafunzi litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 104 na kuipongeza kampasi hiyo kwa juhudi zinazoendelea za utunzaji wa mazingira.



Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya Magavana wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt. Lulu Mahai ametoa wito kwa wadau wa malezi na makuzi kutumia Taasisi ya Ustawi wa Jamii kupata taaluma hiyo.

"Tunalishukuru shirika la SOS Village kwa kushirikiana na taasisi kuwaandaa walezi wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto hasa kwa kutambua kuwa taasisi ya ustawi wa Jamii ni taasisi pekee ya Serikali inayotoa kozi hiyo" amesema Lulu Mahai.

Ameongeza pia taasisi inaendelea na ujenzi wa hostel na maktaba ili kuongeza udahili.



Naye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya amesema Taasisi hiyo imekuwa na manufaa kwa wilaya hiyo kutokana na kuendelea kupanuka kitaaluma hivyo watakuwa msaada mkubwa kwenye jamii..

"Tumekuwa na siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo waathirika wakubwa na wanawake na watoto, kundi hili ni askari wako watakaotusaidia katika juhudi za kupambana na ukatili wa kijinsia, mkitoka hapa tunatarajia mkatusaidie kwenye jamii" amesema Mwaipaya.

Baadhi ya wahitimu wamesema wameshukuru kupata mafunzo katika fani za Ustawi wa Jamii katika malezi na makuzi pamoja na ufundi ambapo wametoka na ujuzi utakaowasaidia kuangalia fursa kupitia changamoto zilizopo kwenye jamii.

Katika mahafali hayo ya tano, jumla ya wahitimu 247 wametunukiwa astashahada na stashahada katika fani ya Ustawi wa Jamii, na malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.


Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI