WAZIRI GWAJIMA AYATAKA MABARAZA YA WAZEE KUKEMEA UKATILI KWA WAZEE


 Na WMJJWM, Kilimanjaro

Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyataka Mabaraza ya Wazee katika ngazi zote kupaza sauti za wazee dhidi ya aina zote za ukatili wanaofanyiwa na jamii. 

Waziri Gwajima ameyasema hayo alipozungumza na Wazee wanaotunzwa katika Makazi ya Wazee Njoro Moshi mkoani Kilimanjaro, alipofika kuwasalimia Desemba 15, 2022.

Amewataka Maafisa Ustawi na Maendeleo kuhakikisha Mabaraza ya Wazee kote nchini yanaundwa na yanawezeshwa kufanya kazi kwani kupitia Mabaraza hayo, haki na usalama wa Wazee vitaimarika.

Aidha amekemea baadhi ya watu wenye tabia ya  kuwahukumu Wazee kwa tuhuma za ushirikina kuwa waache mara moja kwani Serikali haitavumilia kabisa jambo hilo ambalo ni kinyume na haki za binadamu. 

"Iwapo kuna mtu ana kero na Mzee achukue hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu, sheria na kanuni za nchi na si kujichukulia sheria mkononi" amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima ametumia nafasi hiyo pia kuwapa Salaam za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Wazee ni  kipaumbele cha Serikali ndio sababu  ameunda Wizara inayoangalia Wazee, hivyo kuwataka  wawe na amani.

Aidha, amewapongeza watumishi kwa kazi wanayoifanya ya kuangalia Wazee hao na kuwapatia huduma muhimu zikiwemo chakula na afya.

Akizungumza kwa niaba ya Wazee wenzake, Mzee James Joseph amemuhakikishia Waziri Dkt. Gwajima kuwa wanapata matunzo vizuri kituoni hapo na kuomba kuongezwa kwa idadi ya watumishi pamoja na kupewa bima kubwa za afya. Aidha, Mzee James ametoa shukrani kwa Rais Samia kuwa, wanashukuru kuona maelekezo yake kuwa wazee watembelewe linatekelezwa. 

Makazi ya Wazee Njoro ni moja ya  makazi 14 nchini yanayosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na kwasasa yanahudumia Wazee 18.



Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI