Hayo yamebainishwa leo tarehe 19 Januari, 2023, kwenye Warsha iliyoandaliwa na Taasisi hiyo katika ukumbi wa Chuo cha Utalii, Jijini Dar es salaam.
Akifungua warsha hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Bw.Seka Kasera amesema lengo la kukutana na wadau hao muhimu ni kuendelea kuwakumbusha wajibu wao wa kulinda na kukuza bunifu nchini.
“Leo tumekutana na Wafanyabiashara kwa lengo la kuwakumbusha kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu hasa Alama za Biashara na Huduma (Nembo) na Hataza, ambazo ni huduma zinazotolewa na BRELA.
Ni matarajio yetu kwamba baada ya warsha hii wadau hawa watakuwa na uelewa mpana kuhusu masuala yanayohusu huduma hizo na jinsi ya kutumia katika biashara zao ili kukuza uchumi” ameeleza Bw. Kasera.
Ameongeza kuwa ubunifu katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia umekuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi hivyo wamiliki na wafanyabiashara hawana budi kutumia bunifu zao ili kujikuza zaidi.
Bw. Kasera amezitaja faida za kutumia nembo iliyosajiliwa katika bidhaa ni pamoja na kumpa mfanyabiashara haki ya kipekee kutumia alama husika na kuwazuia wengine kutumia alama hiyo isipokuwa kwa ruhusa au ridhaa yake.
Faida nyingine ni kudhibiti ushindani wa bidhaa au huduma katika soko, kuendeleza umaarufu wa ubora wa bidhaa au huduma, kuhifadhi ulinzi wa alama iliyosajiliwa pamoja na mabadiliko husika.
Pia kumpatia mmiliki wa Alama husika kipato kwa njia ya kuuza Alama au kutoa haki ya matumizi kwa mtu mwingine.
Ametaja faida nyingine kuwa ni kuwawezesha watumiaji wa bidhaa kutambua na kuchagua alama au huduma kutokana na ubora na kumpa mmiliki haki ya kisheria kumchukulia hatua mtu anayeiga alama hiyo.
Naye Afisa Mwandamizi kutoka Idara ya Miliki Ubunifu BRELA, Bw. Raphael Mtalima amewaeleza wadau kuhusu Hataza ambayo ni ni hati inayotolewa na Serikali kwa mvumbuzi kutokana na uvumbuzi alioufanya wa kitu au namna ya kuunda kitu unaolenga kutatua tatizo au kutoa jawabu/ufumbuzi mahsusi katika nyanja ya teknolojia husika.
Aliongeza kuwa Ili uvumbuzi upatiwe Hataza unatakiwa uwe mpya, uoneshe njia ya uvumbuzi na pia uweze kutumika katika eneo husika na usajili wake unafanyika kwa njia ya mtandao.
BRELA inaendelea na utaratibu wake wa kutoa elimu ya Miliki Ubunifu katika sehemu mbalimbali kwa kuandaa warsha na makongamano mbalimbali ili wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo wanufaike na elimu hiyo.
0 Comments