DKT. MOLLEL AELEKEZA USHIRIKIANO BAINA YA HOSPITALI ZA SERIKALI NA ZA BINAFSI KATIKA KUWAHUDUMIA WANANCHI.


Na Mwandishi wetu

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameelekeza Wataalamu wa afya nchini  kuendelea kuimarisha ushirikiano katika utendaji ili kuongeza tija na ufanisi katika kuwahudumia wananchi ili wasipate changamoto yoyote.

Dkt. Mollel ameelekeza hayo alipofanya ziara ya kuangalia hali ya utoaji huduma na utendaji katika hospitali Ruthelani  iliyokuwa ikifanya kazi kama hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Wilaya ya Karatu iliyokamilika na kuanza kutoa huduma hivi punde.

Aidha, Dkt. Mollel amemwelekeza Meneja wa MSD kanda ya Kaskazini kuhakikisha ndani ya mwezi huu Januari analeta vifaa na vifaa tiba na dawa ambavyo fedha yake ipo kwenye akaunti ya MSD ili wananchi wengi zaidi waanze kunufaika na uwekezaji huo mkubwa uliofanywa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Ameendelea kusisitiza kuwa, MSD kutoa kibali cha kuruhusu kituo kununua dawa kwa mshitiri ndani ya saa 24 endapo dawa hizo hazitakuwepo kwenye stoo ya dawa ili kuindoa changamoto ya upungufu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma nchini. 

Pia, Dkt. Mollel amesema, Mhe. Rais Dkt   Samia Suluhu Hassan tayari amewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu, dawa na vifaa tiba, hivyo kumwelekeza Mganga mkuu wa Wilaya kusimamia ubora wa huduma kwa wananchi ili kuondoa malalamiko yanayoweza kuzuilika. 

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amemshukuru uongozi mzima wa Wilaya ya Karatu ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Dadi Kolimba kwa usimamizi mzuri wa fedha zilizotolewa na Serikali mpaka kukamilika kwa ujenzi huo wa Hospitali na kuanza kutoa huduma kwa wananchi. 

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Kolimba amesema, amemshukuru Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza jumla ya shilingi Bilioni 2.4 katika ujenzi wa Hospitali hiyo huku fedha nyingine zikitolewa na Wadau, na kuahidi kuendelea kusimamia huduma katika hospitali hiyo ili wananchi wasilalamike. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu Mhe. Daniel Awack ameshukuru uongozi wa iliyokuwa hospitali ya Wilaya kwa namna wanavyo wahudumia wananchi wa Karatu, huku akiweka wazi ataendelea kuishauri Serikali katika kuboresha huduma ili wananchi wa Wilaya hiyo wanufaike.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU