Na Asha Mwakyonde
TAFITI chache zilizofanyika hapa nchini mkoa wa Kilimanjaro na Pwani zinaonesha ukubwa wa tatizo la ugonjwa sugu wa figo kutofanya kazi ni asilimia 7 hadi 13, sawa na wagonjwa 7 hadi 13 kati ya watu 100 wakiwa na ugonjwa huo. Kwa upande wa ulimwengu inakadriwa tatizo hilo kuwa asilimia 7 hadi 16.
Ugonjwa sugu ya figo kutofanya kazi vizuri ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanayohusiana pia na ulaji usiofaa na mitindo mbaya wa maisha.
Athari za Ugonjwa huo ni kubwa kwa kuwa matibabu yake ni ghali hivyo kinga ndio njia pekee ya kuepuka ugonjwa huo.
Akizungumzia Ugonjwa sugu wa figo kutofanya kazi vizuri Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH),Dk. Kessy Shija ameeleza kuwa kazi kuu ya figo ni kutoa uchafu mwilini, kurekebisha madini mbali mbali, kutengeneza vichocheo vya kutengeneza damu na upatikanaji wa madini ya kalsium mwilini.
Dk.Shija amesema figo ikipata changamoto ya kutofanya kazi vizuri husababisha mwili kubakiwa na uchafu.
Mgonjwa huyo pia anakuwa na upungufu wa damu pamoja na madini ya kalsium. Vile vile anaweza kuvimba kutokana na mwili kushindwa kurekebisha vizuri kiwango cha maji.
SABABU ZA UGONJWA HUO
Dk.Shija amesema sababu za ugonjwa sugu wa figo kutofanya kazi vizuri zipo nyingi lakini mbili ndio zinachangia kwa kiasi kikubwa ambazo ni shinikizo la juu la damu (hypertension) na kisukari (diabetes).
Amesema sababu nyingine ni kutumia dawa zenye madhara kwenye figo huku akitolea mfano dawa za kutuliza maumivu, utumiaji wa dawa za kienyeji.
"Sababu nyingine ni kuziba kwa mfumo wa mkojo inayotokana na uvimbe kwa wanaume tezi dume na kwa wanawake saratani ya shingo ya kizazi, sababu nyingine ni maambuzi ya wadudu kama vile virusi vya ukimwi, homa ya ini," amesema.
Ameongeza kuwa ugonjwa sugu wa figo kutofanya kazi vizuri husababisha madhara ya kimwili taratibu bila mgonjwa kufahamu. Kuna hatua tano ambazo mgonjwa huyo anapitia ili kufika hatua ya mwisho (hatua ya tano). Katika hatua za awali (1-2) hakuna dalili inayojionyesha kuwa mgonjwa huyo ana ugonjwa sugu wa figo kutofanya kazi vizuri.
Kwa mujibu wa Dk.Shija hatua ya tano ni hatua ambayo mgonjwa anakuwa na hali mbaya kwa kuwa uwezo wa figo kufanya kazi ya kutoa uchafu mwilini iko chini hivyo mgonjwa anaathirika kutokana na uchafu kulundikana mwilini.
Vile vile anakuwa na upungufu wa damu, mifupa kuwa milaini na pia anaweza kuwa amevimba kutokana na kutokojoa vizuri kwani figo zinakuwa na uwezo wa chini wa kiutendaji.
"Dalili atakazokuwa nazo na ugonjwa
Kuchoka, kuwashwa mwili, kutapika chakula chote anachokula mgonjwa. Vyote hivyo vinatokana na mlundikano mkubwa wa uchafu mwilini .
Vile vile anaweza kuwa na upungufu wa damu au kuwa na maji mengi kwenye mwilini inayosababisha kuvimba na kupumua kwa shida pamoja na kwenye mapafu, ,"ameeleza Dk. Shija.
MATIBABU
Daktari huyo ameeleza kuwa mgonjwa akifikia hatua hii (hatua ya tano) lazima apatiwe matibabu ya kuondoa taka zilizolundikana mwilini na bila ya matibabu hayo anaweza kupoteza maisha.
Dk.Shija amefafanua kuwa matibabu hayo hapa nchini ni kuchuja damu kwa njia ya mashine (haemodialysis) au kupandikiza figo ya mtu mwingine.
"Huduma hizi zote zinapatikana katika hospitali ya BMH na zilianzishwa tangu mwaka 2018 na zimeweza kuhudumia wangonjwa wengi kutoka mikoa mbalimbali hasa katika kanda ya kati kwa upande wa uchujaji damu na nchi nzima katika upandikizaji figo," amesema.
CHANGAMOTO
Akizungumzia kuhusu changamoto za matibabu Dk.Shija ameeleza kuwa ugonjwa huo unahitaji matibabu ya maisha kwa anayechuja damu na aliyepandikizwa figo hivyo kufanya matibabu haya kuwa ya gharama kubwa.
Dk. Shija amesema ili kuepuka visabishi vya ugonjwa huo anashauri wananchi kutumia njia ya kinga badala ya kutibu hivyo anahamasisha kufuata mitindo mizuri ya maisha ikiwemo kufanya mazoezi, kuepuka kutumia madawa bila maelekezo ya Wataalamu wa afya pamoja na kuepuka uzito uliopindukia.
Kwa wale wenye magonjwa tayari ya shinikizo la juu la damu au kisukari wahakikishe wanafuata ushauri wa watalaamu ikiwa ni kudhibiti ugonjwa kuleta madhara ya kwenye viungo kwa kudhibiti shinikizo la juu la damu na sukari kwa kuwa na viwango vinavyotakiwa mwilini.
0 Comments