Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akiwaongoza watumishi kumkaribisha Dkt. John Jingu leo Machi 06, 2023 baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo hivi karibun.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo mara baada ya kuwasili ofisini kwa mara ya kwanza leo Machi 06, 2023 baada ya kuteuliwa hivi karibuni
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, Waziri Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo mara baada ya kuwasili na kupokelewa ofisini kwake Dodoma, tarehe 06 Machi, 2023.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJW
Na WMJJWM, Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amewahakikishia Wanawake nchini kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Wadau itaendelea kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha Wanawake kutumia Teknolojia na huduma za Kidigitali ili kujikwamua Kiuchumi.
Waziri Gwajima ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake jijini Dodoma leo Machi 06, 2023 katika kuelekea Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 08 kila Mwaka.
“Mwaka 2020 mafunzo ya uendeshaji na ufundishaji wa TEHAMAyalitolewa kwa wakufunzi 1347 ambao wanaume 893 na wanawake 454, vilevile Serikali inawekeza katika ujenzi Barabara, Miundombinu ya Maji,Afya ,kilimo,ufugaji na Sekta zote ambapo uwekezaji huo ni nguzo kubwa katika kukuza Uchumi.”Amesema Dkt Gwajima.
Dkt Gwajima amesisitiza Wanawake kutumia Majukwaa ya uwezeshaji Kiuchumi yaliyoundwa kwenye ngazi zote katika mikoa 12 hadi sasa, ili kunufaika na fursa za Uwezeshaji zinazotolewa na Serikali pamoja na Wadau wengine.
Ameongeza kuwa maadhimisho ya siku ya Wanawake Mwaka huu nchini yatafanyika katika ngazi za Mikoa kwa kuratibiwa na viongozi wa Mikoa, ambapo kaulimbiu ni "Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia:Chachu katika kufikia usawa wa Kijinsia"
Awali Waziri Dkt. Gwajima amewaongoza Watumishi wa Wizara hiyo kumkaribisha Katibu Mkuu Dkt John Jingu baada ya kuwasili kwa mara ya kwanza Wizarani hapo tangu kuteuliwa kwake ambapo amesema anatumaini uzoefu aliopata utasaidia kuwa Chachu ya utendaji kazi ndani ya Wizara na kuwataka watumishi kushirikiana daima.
"Wizara hii ina majukumu mengi na mazito ikiwemo kuhakikisha kwenye jamii Sera za Wizara zote zinafahamika na jamii zinatekelezwa kikamilifu" amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake Dkt. Jingu akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo amesisitiza juu ya ushirikiano wa hali ya juu baina ya Watumishi ili kufanikiwa katika kufikia malengo ya Wizara.
“Katika mambo yote nataka tufanye kazi kama Timu ili matokeo Chanya yaonekane. Tufanye kazi kwa ufanisi kwa kutumia Rasilimali zilizopo ili kupata Matokeo yanayotarajiwa” amesema Dkt Jingu.
Naye Mkurugenzi Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Wizara amemuahidi Katibu Mkuu Jingu ushirikiano na ufanisi katika kutekeleza majukumu.
0 Comments