VIJANA WATAKIWA KUHAKIKISHA NCHI ZA AFRIKA ZINAJIKOMBOA KIUCHUMI


 Na Mwandishi wetu, Pwani

KATIBU wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa(SUKI) Mbarouk Nasoro Mbarouk,amewataka vijana kutoka katika vyama vya wapigania uhuru kusini mwa Afrika, kutumia mafunzo watakayo pata katika Shule ya Uongozi ya Kibaha mkoani Pwani,kuleta mabadiliko na matokeo chanya katika vyama vyao na siasa za Afrika kwa ujumla.

Pia amewataka vijana hao kuhakikisha nchi za Afrika zinajikomboa na kuwa huru kiuchumi, kwani bila ya kufanya hivyo mataifa yanaweza kuyumba.

Mbarouck aliyasema hayo jana Kibaha Mkoani Pwani wakati akifungua programu ya mafunzo ya viongozi vijana , kutoka vyama sita vya wapigania uhuru wa Nchi za Kusini mwa Afrika,yatakayofanyika kwa siku 14 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere kuanzia Machi 27 hadi Aprili 7 mwaka huu.

Pia amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitahakikisha kinaendelea kutoa ushirikiano kwa vyama vya siasa vinavyofika chuoni hapo, katika kuhakikisha vinafikia malengo, na kuendeleza dhamira yake ya kujenga umoja na mshikamano katika siasa.

“Mafunzo haya ni mwendelezo wa kujenga umoja na mshikamano na yatasaidia kuongeza uwezo kwa vijana katika kuleta mabadikiko katika nchi za Afrika,

“Vyama hivi vilifanya kazi kubwa kuhakikisha nchi zinapata uhuru, hivyo hivi sasa ni wajibu wa vijana kuhakikisha tunajikomboa kiuchumi, tunapata uhuru wa kiuchumi ,kwani bila kuimarika kiuchumi mataifa yetu yanaweza kuyumba,”alisema 

Aidha Mbarouck alisema, kupitia mafunzo hayo yatawasaidia vijana kuongeza uwelewa, kuleta matokeo chanya katika uongozi na kuongeza kujiamini katika kutekeleza majukumu yao.

Pia aliwapongeza vijana hao kwa kuchaguliwa na vyama vyao , kwasababu kupitia mafunzo hayo watatoa fursa ya kukaa pamoja na kubadilishana uzoefu na kuhakikisha vyama vinaimarika.

Pia alisema programu hiyo ni ya kwanza kwa mwaka 2023 na kwamba tangu kufunguliwa kwa shule hiyo Februari mwaka jana kumekuwa na matokeo mazuri.

Naye Mkuu wa Shule hiyo Profesa Macelina Chijoliga, alisema vijana waliyofika katika mafunzo hayo wapo 96 na watakaa kwa muda wa wiki mbili.

Pia alisema moja ya mambo watakayofundishwa ni uzalendo kwa nchi zao, uadilifu na mambo yatakayofanikisha ushindi katika vyama vyao wakati wa uchaguzi.

Kwamujibu wa Profesa Chijoliga , vijana katika nchi zote sita mataifa yao yanaelekea katika uchaguzi mkuu, hivyo baada ya mafunzo hayo anaamini watenda kusababisha ushindi kwa kubeba bendera za vyama vyao.

Aidha Mkuu huyo wa Shule alisema ,katika mafunzo hayo vijana watafundishwa na viongozi wazoefu, akiwemo Mwanasiasa mkongwe Stephen Wassira, Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu Philip Mangula na mwanasiasa mkongwe Willson Mukama.


Naye Mjumbe wa Halimshauri Kuu ya CCM taifa Dk. Fenela Mkandala, alisema mafunzo hayo ni muhimu katika kujenga misingi imara ya kupata viongozi na wanachama bora wanaoshughulika na wananchi.

Pia alisema vijana wanapaswa kuzingatia mafunzo wanayopata, kwasababu yatawasaidia kuwajengea uwezo na kuleta ushindi katika vyama vyao.

Vyama vinavyoshiriki mafunzo hayo ni MPLA kutoka nchini Namibia, ZANUPF nchini Zimbabwe, FRELIMO Msumbiji, SWAPO nchini ANGOLA, ANC nchini Afrika Kusini na Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU