Na Asha Mwakyonde, Dodoma
SERIKALI Tanzania imetoa msaada wa huduma mbalimali za kibinadamu zikiwamo chakula na Helkopta mbili kuisaidia nchi ya Malawi kutokana na nchi hiyo kupata dhoruba ya kimbunga kiitwacho Tropiki Freddy ambacho kimetokea Machi 13, mwaka huu na kusababisha vifo, kuharibu miundombinu,nyumba, mazao na athari nyingne.
Akizungumza jijini Dodoma leo Machi 18,2023, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Luteni Kanali Gaudentius Ilonda ameeleza kuwa Jeshi hilo limepewa jukumu la kushiriki bega kwa bega kulepele msaada huo.
Luteni Kanali Ilonda amesema kufuatia jukumu hilo Mkuu wa Majaeshi Jacob Mkunda ametoa maelekezo yanayoratibiwa na Mkuu wa Jeshi hilo Luteni Jenarali Salum Haji Othman.
Ameeleza kuwa magari ya JWTZ zaidi ya 37 yataondoka Dodoma muda wowote kupeleka msaada huo nchini Malawi huku akiwataka wananchi kutokuwa na taharuki pindi wanapoyaona magari hayo.
"Baadhi ya magari yatayopelekwa Malawi ni pamoja na gari la wagonjwa (ambulance), karakana ya magari inayotembea (Mobile Workshop) na malori 20 makubwa yenye uzito wa tani 30, na malori 10 yenye uzito wa tani Zaidi ya 18," amesema Luteni Kanali Ilonda.
Luteni Kanali Ilonda amefafanua kuwa magari hayo yatasafirisha mahema,mablanketi, chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu ambayo yametolewa na serikali ya Tanzania.
Ameongeza kuwa Tanzania imetoa tani 1000 za unga wa mahindi ambapo kila siku zitaenda tani 90 kutoka Dodoma na tani 60 kutoka Iringa.
0 Comments