WACHIMBAJI WA MADINI WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI ZA USALAMA MIGODINI


 Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa akiangalia sehemu ya eneo ilipotokea ajali ya wachimbaji wadogo 8 na kufariki baada ya wachimbaji kukutwa na maji ndani ya mashimo wakiwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji mkoani Geita.


Wachimbaji wadogo wa madini wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa (haupo pichani), alipotembelea na kuzungumza nao katika kijiji cha Igando ilipotokea ajali ya wachimbaji wadogo 8 na kufariki baada ya wachimbaji kukutwa na maji ndani ya mashimo wakiwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji mkoani Geita.

Na Mwandishi wetu, Geita

SERIKALI imewataka Wachimbaji wa Madini kuzingatia Kanuni za Usalama na kufuata Sheria na Taratibu za Uchimbaji ili kuepusha ajali katika maeneo ya uchimbaji.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa Machi 17, 2023 alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji katika eneo la ajali ya wachimbaji wadogo waliofunikwa na kifusi na kufariki eneo la Igando Kata ya Magenge Tarafa ya Butundwe Mkoani Geita.

Dkt. Kiruswa, ameiagiza Tume ya Madini kutoa elimu ya Sheria ya Madini hususan elimu ya usalama kwa wachimbaji wanaozunguka maeneo ya uchimbaji katika kipindi cha mvua na kuchukua tahadhari.

"Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inatoa pole kwa wananchi waliopoteza ndugu na marafiki katika ajali hii. Tunawataka wachimbaji mzingatie sheria zilizowekwa na Serikali ili mfanye shughuli zenu kwa tija," amesema Dkt. Kiruswa.

Aidha, amewataka wachimbaji katika eneo hilo kushirikiana na Serikali na mkoa kuchukua hatua kwa wachimbaji wote watakaobainika kukaidi maelekezo ya Serikali kwa wote wanaofanya uchimbaji kwenye maeneo yaliyokatazwa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewataka wachimbaji katika maeneo yenye uwekezaji kutoa ushirikiano kwa watu wenye leseni ya madini ili wafanye shughuli zao bila usumbufu. Amewataka pia kuzingatia usalama katika kazi zao.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita Mhandisi Martin Shija amemuelezea Dkt. Kiruswa kuwa, hatua mbalimbali zilichukuliwa kabla na baada ya ajali. Amesema mmiliki wa leseni na Serikali ya kijiji waliweka walinzi shirikishi  kwenye eneo hilo ili kuzuia uchimbaji haramu na kuepusha madhara.

"Baada ya ajali tumeimarisha ulinzi katika eneo hilo, tumeendelea kufanya kaguzi mara kwa mara ili kubaini kama kazi zinaendelea na kuchukua hatua pale dosari inapojitokeza," amesema mhandisi Shija.

Naye, mwekezaji wa eneo hilo lenye leseni ya utafiti Abdul Stanslaus amesema katika eneo hilo ameendelea kuwa na mahusiano mazuri na jamii katika eneo hilo. Ameomba Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu Sheria ya Madini ili wachimbaji wanaozunguka maeneo ya uchimbaji kuwa na uelewa mkubwa.

Naibu Waziri amefanya ziara baada ya wachimbaji wadogo 8 kufariki tarehe 10 Machi, 2023 baada ya kutokea ajali ya wachimbaji kukutwa na maji ndani ya mashimo wakiwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji.


Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU