Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WAZAZI,walezi wameshauriwa kuwasajili watoto kama wategemezi wao kwenye bima ya afya au kuwasajili kupitia shule wanazosoma lengo likiwa ni kuongeza wigo wa wanachama katika mfumo wa bima ya afya kuelekea bima ya afya kwa wote na kuhakikisha wanachama katika makundi hayo wanajiunga kama familia,kaya au makundi ya wanafunzi kupitia shule Zao.
Ushauri huo unatokana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF),kufanya maboresho ya utaratibu wa usajili na huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa Mpango wa bima ya Afya ya "TOTO AFYA KADI"
Akizungumza Jijini Dodoma Machi 14, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bernard Konga wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu maboresho hayo amesema kuwa uzoefu wa miaka 7 wa kulihudumia kundi hili la watoto kupitia utaratibu wa TOTO AFYA KADI umewezesha Mfuko kufikia watoto 210,664 walio chini ya miaka 18 na umepelekea Mfuko huo kujifunza mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa kati ya mambo ambayo wamejifunza ni pamoja na usajili wa mtoto mmoja mmoja kuchelewesha utekelezaji wa dhana ya bima ya afya ambayo inataka watu kujiunga kwa wingi wao
Aidha ameongeza kuwa mfuko huo umeendelea kushirikiana na shule za Sekondari na msingi ili kusajili wanafunzi na mwitikio unaonesha ndio njia sahihi na pekee ya kuendelea nayo kuhakikisha watoto wengi zaidi wanasajiliwa na kunufakia na bima ya afya.
"Mpango wa Toto afya kadi ulianza rasmi mwaka 2016 baada ya kufanyiwa upembuzi na lengo ikiwa ni kuwajumuisha watoto kupitia shule zao nia ni kufikia kundi kubwa la watoto walio chini ya miaka 18 ambao kitakwimu ni zaidi ya nusu ya wananchi wote ili kufikia azma ya serikali ya watu wote kuwa na bima ya afya(sensa ya 2022 inaonesha watoto chini ya miaka 18 ni asilimia 31 ya wananchi wote)," amesema.
0 Comments