CHUO KIKUU MZUMBE CHAONESHA MFUMO WA 'WATER TANK SYSTEM' UTAKAOSAIDIA JAMII KUTUNZA MUDA


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

MWANAFUNZI  wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu Mzumbe Morogoro, Frank Philimon amebuni mfumo 'Water tank system' unaotumia teknolojia  ambao unatumika katika tenki la maji kutoa taarifa pindi maji yanapojaa na kuisha kwenye tenki hilo.

Mfumo huo ambao unatumia teknolojia ya kisasa umewekewa laini ya simu ya mkononi unatumika kutoa taarifa endapo maji yamejaa kwenye tenki, kuisha na hata kama tenki hilo limepasuka linatoa taarifa ya ujumbe kupitia simu.

Akizungumza jijini Dodoma Aprili 26 kwenye maonesho ya wiki ya Ubunifu Kitaifa (IWTZ), ambayo yanaendelea katika viwanja vya Jamuhuri yenye kaulimbiu isemayo 'Ubunifu kuchangia Uchumi Shindani '  Philimon ameeleza kuwa lengo la kubuni mfumo huo ni kutokana na wanawake kupata changamoto ya kutumia muda mwingine kusubiri tenki la maji lijae huku akishindwa kuendelea na majukumu mengine.

Philimon amesema  matenki yanayotumika kuweka maji ni meusi na maji yakiisha mtu hawezi kujua hadi akatingishe na kwamba mfumo huo hauhitaji kutingisha tenki na badala yake maji yakiisha mhusika atapata ujumbe kwenye simu yake ya mkononi na pia unajiwasha wenyewe na kuzima kama maji yamejaa kwenye tenki hilo.

Ameongeza kuwa mfumo huo unatumia umeme na kwamba lengo la kubuni mfumo wa Water tank system ni kuwarahisishia wanawake ambao ndio wanaofanya kazi ya kujaza maji ambapo wanatumia muda mwingi kuangalia, kusimamia wakati wa kujaza maji.

" Mfumo huu Water tank  system unawafaa sana wamiliki wa hoteli wanaweza kuwa na matenki matano na akajua kila moja changamoto yake mfano tenki namba moja limepasuka mfumo unatuma ujumbe," amesema mwanafunzi huyo.

Amesema mfumo huo ameutengeneza  kwa muda wa mwaka mmoja na nusu hadi kukamilika huku akisema baadhi ya vifaa vilivyotumia alikuwa akiaagiza kutoka nchini China.

Philimon amewataka vijana wenzake wanaohitimu chuoni hapo kuwa elimu wanayoipata waifikishe kwenye jamii kwa lengo la kuisaidia katika changamoto zinazowakabili.

Akizungumzia changamoto alizokutana nazo wakati akifanya utafiti   wa awali  amesema jamii haina uelewa wa masuala ya kufahamu nini maana ya utafiti kwani imekuwa ikiona kama inachunguzwa maisha yao  na pengine haitoi  ushirikiano unaoleta uhalisia wa jambo fulani.


Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA