Na Asha Mwakyonde, Dodoma
VIJANA wameshauriwa kujiingiza katika ujasiriamali ambao utawasaidia kujikwamua kiuchumi badala ya kusubiri ajira za kuajiriwa serikalini ambapo serikali ikiona jitihada zao itaweza kuwashika mkono.
Akizungumza jijini Dodoma Aprili 27,2023, kwenye maonesho ya wiki ya Ubunifu Kitaifa (IWTZ),yenye kaulimbiu isemayo 'Ubunifu Kwa Uchumi Shindani' ambayo yanaendelea kufanyika katika viwanja vya Jamuhuri, Mkurugenzi Mtendaji wa Mvinyo wa Elite 'wine', unaotengenezwa na nyanya mkoani Iringa, Angelina Sylvester,
Amesema lengo la kutengeneza Mvinyo huo kwa kutumia nyanya ni kuwainua wakulima kupitia zao hilo.
Ameeleza kuwa shughuli zao wanazifanya kwa kushirikiana na wakulima kama sehemu ya kutanua wigo wa soko la zao la nyanya kwa kuwa Mkoa huo unazalisha zao hilo ambapo linapotea kwa kukosa soko la uhakika.
"Tupo hapa kwenye wiki ya Ubuntu kitaifa tumekuja kuonesha shughuli zetu za kiubunifu," amesema Mkurugenzi huyo.
"Naishukuru wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia wadau wa maendeleo kama Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kupitia Mamlaka hii iliweza kuleta mradi wa kuendeleza ujuzi (SDF) unashirikiana na vituo mbalimali vya kutoa mafunzo nimepata mafunzo na nimeweza kumiliki kiwanda," amesema.
Ameongeza kuwa kupitia mradi wa SDF ameweza kupata mafunzo ya usindikaji wa vyakula ambapo ulimsaidia kuanza usindikaji huo na kutimiza ndoto zake alizokuwa akizitamani kwa muda mrefu
Ameongeza kuwa ametoa ajira za kudumu kwa vijana wenzake wawili na wengine wanafanya kazi za muda mfupi ambapo wanalipwa na kuongeza.
Akizungumzia changamoto Angelina amesema wanazalisha Mvinyo huo lakini hawana sehemu ya kuuzia bidhaa zao ili Watanzania waweze kuzifahamu huku akisema Mvinyo huo bado ni mpya sokoni.
Afisa Habari na Uhusiano kutoka TEA, Eliafile Solla amesema mamlaka hiyo ni taasisi ya serikali ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na ilianzishwa kwa sheria ya Bunge ya Mfuko wa Elimu Namba 8 ya mwaka 2001 chini ya kifungu 5 (1), ili kuratibu na kusimamia mfuko huo.
Amesema Kisheria TEA inasimamia Mfuko wa elimu wa Taifa ambao umejikitka katika kusaidia jitihada za serikali za kusimamia upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa kote nchini.
Afisa huyo ameongeza mamlaka hiyo ilipewa jukumu la kusimamia mfuko kuendeleza ujuzi mwaka 2017 na kwamba kupitia mfuko huo TEA inashiriki maonesho ya wiki ya Ubunifu Kitaifa.
"Kupitia mfuko huu wa kuendeleza ujuzi TEA inasimamia na kutoa ruzuku kwa taasisi za mafunzo ya ujuzi, na kupita mfuko mamlaka inatoka ruzuku hizi kwa vijana na Watanzania mbalimali na kuweza kuhudhuria mafunzo ya ujuzi ambayo yatawasaidia kutengeneza bidhaa," amesema.
Ameeleza kuwa katika banda la mamlaka hiyo wamekuja na baadhi ya wanufaika ambao wamepata mafunzo ya ujuzi kupitia mfuko huo lengo ni kuuthibitishia Umma wa Watanzania kwamba ujuzi unaweza kuzalisha ajira.
0 Comments