'MAKE UP' ILIVYOMVUTIA KUFANYA KAZI MOCHWARI, AWATOA HOFU WANAWAKE


Na Asha mwakyonde

WATU wengi wanajiuliza kwanini nafanya kazi katika kitengo cha Kuhifadhia Maiti ‘mochwari’ ikiwa mimi ni mwanamke, haya ni  maneno ya Mhudumu wa kitengo hicho 
kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Veronica Mselela (23),wakati wa mahojiano maalumu.

Mselela amesema kufanya kazi mochwari hakuna changamoto wala ushirikina na kwamba  habari zote zinazosikika mitaani ni za kufikirika.

Ameongeza kuwa amefanya kazi katika kitengo hicho zaidi ya mwaka mmoja na nusu na kwamba hajawahi kuona kitu chochote cha kishirikina kama jamii inavyodhani.

Mhudumu huyo amefafanua kuwa habari zinazosikika mitaani ni namna jamii inavyofikiria ugumu  wa kufanya kazi katika kitengo hicho huku akisema watu sio kwamba wanaogopa mtu aliyefariki bali wao ndio wanaogopa kupoteza maisha.


"Kitu kingine ambacho watu wanaogopa, kupata hofu ni sehemu ambayo imehifadhiwa miili mingi lazima wawe na hofu nayo, hapa hakuna mambo ya kichawi wala ushirikina," amesema Mselela.

Kwa mujibu wa Mselela nafanya kazi hii kwa sababu naipenda na nimeisomea nimekuwa nikiona namna mwili unavyoandaliwa na akiwa ni mwanamke mkristo anavyorembwa kwa kupakwa Meka up nikapenda zaidi.

ANACHOJIVUNI

Mselela amesema anachojivunia kufanya kazi katika kitengo hicho ni upekee (unique), kwani sio wanawake wengi wanaoipenda kuifanya kazi hiyo.

Amesema watu wakisikia mwanamke anafanyakazi hiyo wanatamani kumfahamu hicho ndicho anachojivunia pia.

JAMII INAYOMZUNGUKA

Akizungumzia jamii inayomzunguka amesema jirani, ndugu  na marafiki hakuna  anayemtenga kwa kuwa anafanya kazi hiyo wanamuona ni wa kawaida.

Mselela amesema familia yake inajivunia kufanya kazi katika Kitengo hicho ikiwa ni mwanamke pekee kati ya wafanya kazi wengine na kwamba inampa moyo wa kuendelea kufanya kazi hiyo.


WITO WAKE KWA WANAWAKE

Amewataka wanawake kuacha woga na badala yake wafanye kazi hiyo kwani ni kazi kama zilivyokazi nyingine ngumu zinazofanywa na wanawake ambazo ni za wanaume.

Mselela ametolea mfano wanawake wanajihusisha na michezo ya ngumi, kusukuma mikokoteni, kuzibua vyoo na kupaka nyumba rangi huku akisema hizo ni kazi ngumu lakini wanazifanya ili kujiingizia kipato.

Ameongeza kuwa kufanya kazi katika kitengo cha kuhifadhia maiti ni moja ya kipengele kwenye sekta ya afya na kama mwanamke anatamani kufanya kazi kitengo hicho asisikilize maneno ya watu mitaani.

"Tangu nimeanza kufanya kazi hapa sijawahi kuona maiti imeamka au imeongea, sijawahi kusikia mwili umeletwa haujafa haya ni maneno ya wanajamii," ameeleza Mselela.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA