PROF. NDALICHAKO: AJALI 4,993 ZIMETOKEA MAHALI PA KAZI KIPINDI CHA MIAKA MITATU

Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

TAKWIMU za kidunia zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani mwaka 2022 zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 2.9 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi huku zikionyesha kuwa zaidi ya wafanyakazi zaidi ya milioni 4 huumia wakiwa kazini.

Hali hiyo huwafanya  kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu hadi hapo watakapopona.

Hayo yameelezwa jana jijini hapa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana,Ajira, na Wenye Ulemavu  Prof.Joyce Ndalichako wakati akizungumza na waandishi kuhusu maadhimisho ya Usalama mahala pa kazi yanayofanyika April 28 yakila mwaka.

Profesa Ndalichako alisema, kwa upande wa Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249. Katika ajali hizo, vifo vilikuwa 217 huku akisema takwimu hizo ni kubwa sana.

"Takwimu hizo ni kubwa sana zinaathiri utendaji kwa kuwa zinasababisha upotevu wa maisha ya Wafanyakazi na pia kuathiri shughuli wakati wafanyakazi walioumia wakiendelea kupata matibabu. Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kwamba suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi linahitaji jitihada za makusudi katika kukabiliana nalo,"alisema Prof.Ndalichako na kuongeza kuwa

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa kulinda Nguvu Kazi ya Taifa. Kupitia Taasisi yake ya OSHA

Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 miongoni mwa wadau na Watanzania wote kwa ujumla. Lengo ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kazi Nchini yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi," 

Ambapo Prof.Ndalichako amesema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa Mkoani Morogoro katika viwanja vya Tumbaku Aprili 28,2023 na Lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha na kuweka mazingira salama katika sehemu za kazi miongoni mwa wadau.

 "Kauli mbiu hiyo inatokana na Azimio la Wanachama wa Shirika la kazi Duniani (ILO) katika kikao cha Juni 2022 kilichofanyika huko Geneva Uswisi, na kuamua kuwa suala Usalama na Afya mahali pa kazi liwe mojawapo ya Kanuni na Haki tano za msingi kwa wafanyakazi mahali pa kazi,".


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema kuwa moja kati ya eneo ambalo ajali nyingi zinaripotiwa ni katika sekta ya Uzalishaji ambapo imeajiri vijana wengi huku wengine wakiwa hawana ujuzi wa kutosha katika nafasi wanazofanyia kazi.

"Ukweli ni kwamba eneo la Uzalishaji lina matukio mengi ya ajali na hii ni kutokana na vijana wengi kujikita katika eneo hilo kujiajiri ama kuajiriwa huku wengine wakifanya tu bila kuwa na ujuzi wa kutosha au taaluma kwani eneo hilo mara nyingi wanaangalia nguvu sana kuliko taaluma ndio maana ajali zinakuwa nyingi," alisema Mwenda

Mwenda alisema kuwa OSHA imejipanga vyema kuelekea maadhimisho hayo ya 19 ambapo washiriki wote watapatiwa Mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye ulemavu.

"Pia OSHA tutajikita katika kutoa mafunzo kwa Sekta binafsi na zile zisizo rasmi kwa sababu wengi hawapo kwenye mfumo jambo ambalo linawafanya kuwa katika mazingira hatarishi na kufanya kazi bila kuzingatia sheria za usalama na afya mahali pa kazi,"amesema Mwenda.

Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ilianza mwaka1996 Nchini Marekekani Katika Jiji la New York, ambapo waathirika wa watu walioumia na kupoteza maisha wakiwa kazini hukumbukwa. Maadhimisho hayo yalikuwa yakifanywa na Chama Cha Wafanyakazi Duniani. Ilipofika mwaka 2001,Shirika la Kazi Duniani liliona kuwa ni busara kubadilisha madhumuni ya siku hiyo na kuiita “Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani”.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA