Na Asha Mwakyonde,Dodoma
VIJANA hasa wa kike wameshauriwa kutochagua kazi za kufanya na badala yake wafanye kutokana na fani walizojifunza bila kujali ugumu wa fani husika kwa lengo la kujikwambia kiuchimi.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma katika maonyesho ya wiki ya Ubunifu 2023 na wanafunzi wahitimu Wanawake wachomeleaji kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Chuo Cha VETA Dodoma Hilda Mwajombe na Paulina Chuma ambao wamejikita katika utengenezaji wa samani za kuchomelea kama vile vitanda pamoja na utengenezaji wa majiko yanayotumia nishati kidogo ambayo yamelenga kwenye uhifadhi wa mazingira.
Wamesema kuwa wameamua kujikita katika fani hiyo baada ya kuona fursa ya ajira kwenye eneo hilo pamoja na kumuunga mkono Rais Dk. Samia ambaye amonyesha ujasiri kwa namna anavyoingoza nchi.
Kwa upande wa Paulina amesema,licha ya kutengeneza samani za uchomeleaji pia wamebuni majiko yanayotumia mkaa na kuni kidogo ili kunusuru misitu inayokatwa kwa kiasi kikubwa ili kupata nishati hizo.
“Majiko haya yanarahisisha mapishi hasa kwa taasisi kwani yanatumia nishati kidogo,lakini tumebuni jiko ambalo linapika juu na chini ,ambapo eneo la chini linatumika kama ovena,lakini jiko hili linaweza kubadilishwa na kutumia gesi,mkaa,kuni na umeme.”amesema Paulina
Aidha Paulina amesema,kama wanawake wameamua kujikita kwenye fani ya uchomeleaji baada ya kuona kuna fursa ambayo wanawake wengi wameikimbia kwa dhana potofu kwamba hiyo ni kazi ya wanaume kutokana na ugumu wake.
Ametumia nafasi hiyo kuwaasa vijana wa kike na wa kiume kutumia mafunzo wanayopata vyuoni katika kutatua changamoto katika jamii lakini pia watajipatia kipato cha kuendesha maisha yao.
0 Comments