WAKALA wa Usajili wa Biashara na leseni (BRELA), imewahimiza wanawake kurasimisha biashara zao BRELA ili kutambulika kisheria.
Wito huo umetolewa tarehe 25 Aprili, 2023 na Afisa Sheria wa BRELA Bi. Neema Nyadzi wakati akitoa elimu kwa Umoja wa Wanawake Wajasiriamali, juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara zao kupitia sajili mbalimbali za kibiashara pamoja na kupata leseni za Biashara Kundi "A" na viwanda, katika ukumbi wa Sabasaba, Jijini Dar es Salaam.
Bi. Nyadzi amesema watakaporasimisha biashara zao itawawezesha kupata fursa mbalimbali za kibiashara ikiwa ni pamoja na kupata zabuni na mikopo kutoka taasisi za fedha.
"Nawashauri wanawake wenzangu, kusajili biashara zenu ili zitambulike kisheria na kuchangamkia fursa zilizopo", amesisitiza Bi. Nyadzi.
Bi.Nyadzi ametumia fursa hiyo pia kuwaelekeza namna ya kutumia Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS), kwakuwa huduma zote za BRELA zinatolewa kwa njia ya mtandao.
Kwa upande wake mjasiariamali wa bidhaa za nafaka Bi. Asia Mfaume amepongeza jitihada zinazofanywa na BRELA, kuwapatia elimu itakayowasaidia kuzilinda biashara zao kisheria.
0 Comments