Na Asha Mwakyonde,Dodoma
KICHOCHO ni ugonjwa unaosababishwa na minyoo midogo aina ya Schistosoma au Bilhazia na kuna aina kuu mbili za ugonjwa huo ambazo ni kichocho cha mkojo (Urinary schistosomiasis),na kichocho cha tumbo (Intestinal schistosomiasis).
Kichocho cha mkojo husababishwa na minyoo inayoitwa Schistosoma hematobium ambayo huishi katika mishipa ya damu ya kibofu cha mkojo cha binadamu na Kichocho cha matumbo husababishwa na minyoo iitwayo Schistosoma mansoni ambayo inpatikana katika mishipa ya damu ya utumbo.
Afisa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele Uniti ya Kichocho Mohamed Nyati ameeleza kuwa dalili kuu za ugonjwa huyo wa Kichocho cha mkojo ni kuwepo kwa damu katika mkojo, kujisikia hali ya mwili kuchoka, kuwa na kikohozi kikavu
Pamoja na maumivu ya misuli
Pia amezitaja dalili za ugonjwa huo wa Kichocho cha tumbo ni kuharisha kinyesi chenye damu, maumivu ya tumbo na kuvimba tumbo.
UPATIKANAJI WA HUDUMA
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa huduma kwa ugonjwa wa kichocho katika mpango wa kudhibiti magonjwa haliyokuwa hayapewi kipaumbele Nyati amesema ni hufanya kampeni ya kutoa kingatiba za ugonjwa wa kichocho kwa maeneo ambayo yameathirika zaidi na ugonjwa huo kwa kutoa dawa za Praziquantel kwa watoto wenye umri wa kwenda shule miaka 5 hadi 15.
"Pia kwa wale wagonjwa wanaopata matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya tunatoa dawa hizi," amesema Nyati.
Nyati ameeleza kuwa athari za ugonjwa huo ni kupata choo kikubwa chenye damu na kukojoa mkojo wenye damu na kwamba huathiri ini, figo, wengu, utumbo mkubwa na kusababisha saratani.
Ameongeza kuwa athari nyingne ni kusababisha upungufu wa damu mwilini, pamoja na kuathiri via vya uzazi.
HALI ILIVYO NCHINI
Amesema hapa nchini ugonjwa huo umejawanyika kwa ukubwa wa viwango vya maambukizi, kutoka maeneo yenye maambukizi ya chini hadi maeneo mengine yenye maambukizi ya juu (low prevalence areas to high prevalence areas).
Nyati ameongeza kuwa makundi yote hayo yapo katika hatari ya kuathirika na ugonjwa huo wa Kichocho.
Amesema kiwango cha maambukizi ya kichocho kwa tanzania ni kwango cha kati, maeneo machache ndo yana maambukizi kwa kiwango cha juu zaidi ya asilimia 50.
"Maeneo mengi yana maamhukizi kwa kiwango cha kati, kati ya asilimia 10 hadi chini ya asilimia 50 na maeneo mengine maambukizi ni ya kiwango cha chini ya asilimia 10," ameeleza Nyati.
WITO
Nyati akitoa wito kwa jamii ameita kuacha kujisaidia haja kubwa,ndogo kwenye mabwawa, mito, maziwa na mifereji ya maji na kwamba kwa mtu mwenye ugonjwa huo wa kichocho (cha mkojo (Bilhazia) anapokojoa mkojo hutoka na mayai ya kichocho.
Nyati amefafanua kuwa kwa upande wa kichocho cha tumbo, haja kubwa huwa na mayai ya kichocho ambayo huanguliwa mara tu yanapogusana na maji na vijidudu vilivyo anguliwa huingia mwilini mwa konokono na kuendelea kukua, baada ya wiki tano hutoka na kurudi kwenye maji, ambako huogelea kutafuta mtu aliyepo ndani ya maji na huingia kwenye mwili wa mtu kupitia kwenye ngozi.
Pia amewataka kufanya usafi wa mazingira maeneo yenye maji yaliyotuama ili kuepusha mazaliano ya konokono na usafi wa mtu binafsi (personal hygiene).
0 Comments