Na Asha Mwakyonde, Dodoma
CHAMA cha Mapinduzi (CCM),Mkoa wa Dodoma kimepongenza Katibu Mkuu wa chama hicho Daniel Chongolo kwa ziara ya siku 10 aliyoifanya katika majimbo yote 10 mkoani humo yenye malengo mahususi matatu.
Malengo hayo ni kuwatembelea na kuwasikiliza wananchi kuhusu changamoto zao,kuzitatua papo kwa papo au kuziwekea msukumo wa kupata utatuzi unaokidhi matarajio na matumaini ya watu,kuimarisha uhai wa chama kushiriki mikutano ya mabalozi, mashina ya CCM, kuimarisha ujunzi ofisi zake na miradi ya uchumi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo ambayo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 hadi 2025.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma Juni 27,2023 na Katibu Mkuu wa chama hicho Mkoa wa Dodoma Pili Mbanga wakati akitoa tamko la ziara hiyo ameeleza kuwa, Halmashauri kuu ya CCM ya Mkoa huo ilikutana katika kikao chake cha kawaida cha siku mbili na kutoa tamko hilo la kumpongeza katibu Mkuu huyo.
Amesema katika ziara hiyo karibu Mkuu wa Chama hicho Chongolo amefanya jumla ya mikutano mikubwa 9, ya wananchi na wapenzi wa chama, mikutano 20 ya wananchi kwenye miradi ya chama na serikali na mikutano mingine sita kwenye mashina.
"Katibu Mkuu alikagua na kutembelea miradi 31 ambapo miradi 28 ni ya serikali, miradi mitatu ni ya chama. Kote alikopita katika miradi hii ametoa maelekezo mbalimbali kwa majimbo yote 10 ambapo mengine yamefanyiwa kazi papo kwa papo na mengine alielekeza muda wa kutekelezwa," amesema Katibu wa CCM Mkoa Mbanga.
Ameongeza kuwa katibu Mkuu huyo ameonesha umahiri mkubwa wa kusikiliza, kukagua na kutoa majibu mwafaka papo kwa papo katika sekta za maji, Nishati (umeme),afya, elimu, miundombinu, migogoro ya ardhi au wanyama wakali wanaoharibu mazao na kuhatarisha uhai wa watu.
Mbanga ameeleza kuwa katika kutekeleza maagizo ya katibu Chongolo wizara ya maji imetoa kiasi cha fedha zaidi ya shilingi milioni 281 kukamilisha miradi ya maji Pwaga huko Kibakwe na kutangaza zabuni ya shilingi bilioni 4, lengo likiwa ni kuimarisha upatikanaji wa maji katika Mji wa Mpwapwa ambapo mchakato wake utakamilika ndani ya siku 60.
"Viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Dodoma tumejipanga vilivyo kuendelea kuwa sehemu ya mageuzi makubwa ya kimaendeleo yanayoendelea kushuhudiwa ndani ya uongozi wa awamu ya sita ikiwa ni pamoja na kuendelea kufanya siasa za kistaarabu ambazo ndizo desturi ya Chama Cha Mapinduzi," amesema Mbanga.
Amebainisha kuwa chama hicho Mkoa wa Dodoma kipo imara na kuendelea kuwa na utayari kutekeleza kazi zake na kupokea maelekezo na maagizo yote ya viongozi wa Kitaifa yenye malengo ya kuimarisha chama,kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Mkoa huo, kuleta mashikamano miongoni mwa wanacham, kuibua na kuendeleza miradi mbalimbali ya kiuchimi pamoja na kudumisha mshikamano chanya na wadau wengine mkoani humo .
0 Comments