Bibi Elizabeth Mungure na Bwana Mwarabu Kitisha wakipeana mikono ikiwa ni ishara ya kumaliza mgogoro wao uliodumu kwa muda wa miaka 10 huku wakishuhudiwa na Viongozi wa Kijiji, Wazee wa kimila na wataalam wa MSLAC Mei 30,2023.
Kikao cha usuluhishi wa kesi ya Bibi Elizabeth Mungure na Bwana Mwarabu Kitisha kilichochukua zaidi ya saa nne kikiendelea kijijini Mbigiri, wilayani Kiteto Mei 30,2023.
Na Lusajo Mwakabuku & George Mollel WKS – Kiteto
TIMU ya wataalam wanaotekeleza Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) katika Mkoa wa Manyara, wilayani Kiteto, imefika katika Kijiji cha Mbigiri na kumaliza mgogoro uliodumu kwa miaka 10 kati ya Bibi Elizabeth Mungure na Bwana Mwarabu Kitisha ambao kwa pamoja walikubaliana kumaliza tofauti zao kwa kutoendeleza shauri hilo mahakamani.
Usuluhishi wa Mgogoro huo uliochukua takribani masaa manne ukihusisha viongozi wa Kijiji pamoja na wazee wa kimila ulifanyika siku ya tarehe 30/05/2023 ambapo pande zote mbili zilizokuwa zinavutana ziliridhia kuwa mgogoro huo uishe kwa makubaliano kwamba Mzee Mwarabu aondoke yeye na mifugo yake katika eneo hilo ifikapo Julai 2023 na Bi. Mungure aondoe kesi hiyo mahakamani.
Kesi hiyo licha ya kuchukua muda mrefu lakini pia ilifika hadi ngazi ya Mahakama Kuu na ikaonekana irudi ianze upya katika ngazi ya Kijiji. Wakati hilo likitekelezwa, ndipo kamati ya wataalam wa Mama Samia Legal Aid Campaign ilifika katika Kijiji hicho na Mwenyekiti wa Kijiji pamoja na mambo mengine akawaelezea wataalam hao juu ya mgogoro huo na kuwaomba kuona namna ya kuumaliza.
Kabla ya kuanza kutafuta suluhisho kuhusu mgogoro huo, timu ya wataalam wa MSLAC ilitoa elimu kwa ufupi juu ya umuhimu wa kumaliza migogoro kwa njia mbadala ikiwemo usuluhishi kwani njia hii hutumia gharama ndogo lakini pia hufanyika eneo husika tofauti na keshi inapopelekwa mahakamani ambapo wahusika hulazimika kupoteza muda mwingi kuhudhuria katika kusikiliza mashauri mahakamani muda ambao wangekuwa wakiutumia kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Baada ya elimu hiyo, timu ikafanya ziara ya kukagua mipaka ikiwa na pande zote mbili zenye mgogoro ambapo wakafanikiwa kuongea na uongozi wa Kijiji uliopo na uliotangulia (Wastaafu) na pia wazee wa kimila walioishi eneo hilo kwa muda mrefu ambapo kwa pamoja walifanya majadiliano na mapendekezo yakafanyika yaliyopelekea kumaliza mgogoro huo.
Baada ya pande zote mbili kuridhia suluhisho hilo lililosimamiwa na wataalamu wa MSLAC, wawili hao walishikana mikono ikiwa ni ishara ya kumaliza tofauti zao juu ya huo mgogoro na kuruhusu amani itawale na wazee wa kimila wakiongozwa na mzee wa ukoo bwana Mbembile Oleikurkur wakawaapisha ili wasiendelee na mgogoro huo.
Timu ya MSLAC imekamilisha kazi ya kutoa huduma ya msaada wa kisheria Mkoani Manyara siku ya tarehe 01/06/2023 na inatarajia kuendelea na kazi hiyo katika mkoa wa Shinyanga kuanzia tarehe 12 – 22 ya mwezi wa Julai mwaka huu. Huduma zinazotolewa ni pamoja na elimu ya sheria za mirathi, migogoro ya ardhi, ukatili wa kijinsia, na kutatua kero mbalimbali zinazohusu masuala ya kisheria.
0 Comments