FAHAMU SABABU NGUO ZA KAKI, KIJANI KUVALIWA KATIKA HIFADHI


Na Asha Mwakyonde, Dar es salaam

WANAOTEMBELEA Hifadhi za Wanyama Pori  wameshauriwa kuvaa nguo zinazoendana na kipindi kilichopo ili kutengeneza ufanano wa  mazingira na kusaidia wanyama hao wasishtuke kama kuna kitu kigeni kimeingia katika himaya yao.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam jijini na Mhadhiri Msaidizi wa Masomo ya Utalii kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori -Mweka,Vitales Kabonda katika Maonesho ya 18 Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),ambayo yalianza Julai 17, na kuhitimishwa Julai 22, 2023 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja yenye kaulimbiu isemayo 'Kukuza Ujuzi Nchini kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa Uchumi Imara na Shindani,' ameeleza kuwa hifadhi za wanyama pori mara nyingi zinapitia vipindi vikuu viwili kwa mwaka, kipindi cha ukame na cha mvua nyingi.

Kabonda  amesema kuwa kipindi cha mvua nyingi majani yanakuwa ya kijani hivyo wanaofanya kazi katika hifadhi za wanyama wanavaa mavazi ya kijani.

Amesema kipindi cha ukame mazingira yanakuwa ya rangi ya kaki na kutokana na hali hiyo wanaoongoza hifadhi huvaa nguo zinazoenda na mazingira hayo.

"Kila kipindi kuna mavazi yake hata magari nayo  yanaendana na kipindi kilichopo  kama ni kipindi cha ukame ambapo majani yanakuwa ya rangi ya kaki na magari, mavazi yanakuwa ya rangi hii na hata kipindi cha mvua pia ni hivyo hivyo," ameeleza. 


Ameongeza kuwa hata majengo yanayojengwa kwenye hifadhi za wanyama yanakuwa na rangi ya kijani ili kuleta mfanano wa mazingira na kwamba kipindi hicho kinadumu kwa muda mrefu kuliko kile cha ukame.

Kabonda amefafanua kuwa kipindi cha ukame kinadumu kwa muda wa miezi minne hadi mitano tofauti na kile cha mvua nyingi ambapo kinakuwa miezi saba hadi nane.

Mhadhiri huyo Msaidizi amesema Watembeleaji hawaruhisiwi kushuka kwenye gari wakiwa matembezini katika hifadhi za wanyama pori wanatakiwa kubaki ndani ya gari, mnyama atakachokiona ni ile gari ya rangi ya kaki au kijani.

Ameongeza kuwa kuna maeneo ambayo yametengwa rasmi kwa ajili ya watembeleaji kushuka ambayo wanyama hawafiki kila mara katika maeneo hayo.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI