SUZA:FILAMU YA 'ROYAL TOUR' ILIVYOLETA CHACHU KUONGEZA VIWANGO PROGRAMU

Na Asha Mwakyonde

SERIKALI imekuwa ikiangalia maeneo yenye mvuto ya kuleta wawekezaji pamoja na kupata maeneo ya kuboresha uchumi wa nchi, katika kuhakisha hili Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alitengeneza Filamu ya 'Royal Tour' ambayo imekuwa ni mkombozi wa kuliingizia Taifa kipato kupitia fedha za kigeni.

Uzinduzi wa filamu hiyo ulianzia Marekani Aprili 18 na 21, 2022 katika miji miwili ya New York na Los Angeles  ambapo  nchini  ilizindulia  jijini Arusha Aprili 28, ikifuatiwa na Zanzibar  Mei 7,na kuhitimishwa jijini Dar es salaam Mei 8 mwaka huo.

Baada ya Rais Dk. Samia kutengeneza filamu ya Royal Tour imeiwezesha serikali  kuwa na ongezeko la pato la Taifa kwa asilimia 76.

Filamu ya royal tour imekuwa chachu ya kuongeza nguvu katika kuimarisha programu za Utalii zinazotolewa na Chuo Kikuu Cha Taifa Zanzibar (SUZA), na Mkuu wa Chuo hicho  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali  Mwinyi amekuwa akiwapatia  miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa chuo hicho.

Miongozo hiyo inaenda sambamba na utekelezaji wa sera ya kitaifa ya Uchumi wa Buluu, miongoni mwa sekta hizo ni sekta ya utalii.

Akizungumzia programu zinatolewa na chuo hicho Makamu Mkuu wa SUZA,Profesa Mohamed Makame Haji katika Maonesho  ya 18 ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ambayo yalianza Julai 17, na kuhitimishwa Julai 22, mwaka huu kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja yenye kaulimbiu isemayo 'Kukuza Ujuzi Nchini kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa Uchumi Imara na Shindani', ameeleza kuwa moja ya programu wanazozitoa ni ya utalii.

Prof. Haji amesema awali walikuwa wakitoa programu za Utalii na Ukarimu katika kiwango cha cheti na diploma ambapo kwa sasa Chuo kimeongeza nguvu kwa kutoa programu hizo kwa kiwango cha shahada ya kwanza.

Ameongeza kuwa programu ya Royal Tour ambayo Rais Dk.Samia kwa nafasi yake ameonesha mfano wa kuitangaza nchi nje ya mipaka ya Tanzania.


"Katika hili tunahakikisha tunapata vijana ambao wanaweza kwenda kusimamia vema sekta ya utalii ili iwe na matunda makubwa.Suala la matembezi kwa watu ni la asili na halikuwekwa katika mkakati wa kulinyanyua na kuleta mabadiliko makubwa nchini," amesema.

Kwa mujibu wa Prof. Haji, ikiwa mkuu wa nchi Rais Dk.Samia ameitangaza Tanzania nje sisi tuliobaki lazima tuunge mkono ili tuweke mazingira stahiki, sahihi yatakayoweza kuweka hadhi ya Royal  Tour katika huduma na kazi mbalimbali za masuala ya kiutalii.

Ameongeza kuwa wanataasisi inayosimamia programu ya utalii na ukarimu, kwenye eneo hilo wamekuwa mstari wa mbele kwa kuwa sekta ya utalii hapa nchini imekuwa ikiingiza kipato kikubwa kwa kuingiza fedha za kigeni.

Kwa mujibu wa Makamu huyo wameweza kupata nafasi kubwa kuhakikisha inawatoa vijana ambao wanaweza kushiriki moja kwa moja kusaidia Taifa kupata nafasi ya kuwa na hoteli, shughuli za ukarimu ambazo zinaendeshwa kisayansi.

Prof. Haji amefafanua kuwa kwa sasa wana Skuli 'Schools' 11 ambazo zinafanya kazi ya kutoa elimu, tafiti pamoja na kutoa Ushauri elekezi katika maeneo mbalimbali Kisiwani Unguja na Pemba.

Amesema wamekuwa na uwezo wa kutoa elimu katika ngazi ya cheti Diploma,shahada ya kwanza, shahada ya pili pamoja na uzamivu katika utaalamu wa Kisawahili.

Prof.Haji amesema kuwa wanatoa programu zao katika maeneo ya fani za elimu mbalimbali ikiwamo Elimu Jumuishi ambayo wanawafundisha vijana ili kuwa na uwezo wa kufundisha watu wenye uwezo tofauti, Watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu.

Amefafanua kwamba katika elimu ya msingi, Sayansi na maeneo hayo wamekuwa wakisimama imara kuhakikisha wanazalisha walimu ambao wataisaidia nchi na jamii ili kuwandaa vijana kuwa na misingi iliyobora ya kisayansi.


PROGRAMU ZINAZOTOLEWA SUZA

Prof.Haji ameeleza kuwa wana skuli, shule ya Sayansi jamii na Sayansi ya asili ambayo inatoa programu mbalimbali za Sayansi ikiwamo ya Sayansi ya mazingira, Sayansi ya asili na Sayansi ya jamii ambazo zinahusisha masuala yote ya Baiolojia, Kemia na Fizikia.

Ameongeza kuwa wanaandaa programu ambazo zinakwenda sambamba na mabadiliko na mageuzi ya uchumi waliyonayo lengo likiwa ni kila mmoja anayepita katika programu hizo aweze kuwa na uwezo ambao utamuwezesha kuwa mbunifu na kutumia elimu yake na ujuzi kuongeza maendeleo ya nchi.

Prof. Haji amesema pia wana skuli za biashara, uchumi, ujasiriamali, uongozi wa biashara na katika maeneo ya kilimo ambapo wanatoa fani mbalimbali za kilimo.

Amefafanua kuwa kwenye fani ya lugha wana skull za kiswahili na lugha za kigeni ambayo inafanya kazi ya kutoa taaluma zake katika maeneo ya lugha mbalimbali na kwamba kwa sasa wana lugha tisa znazofundishwa chuoni hapo katika ngazi mbalimbali zikiwamo kiswahili, kiingereza, kijerumani, Kihispania na Kichina.

Prof. Haji ameongeza kuwa wana skuli ya afya ambayo inatoa programu zake tofauti tofauti katika maeneo ya Sayansi za afya ya tiba huku akisema kwamba pia wana skuli za afya ya meno na kinywa ambayo inatoa programu za diploma na degree katika Sayansi ya meno na Afya ya kinywa.

Pia amesema wana skuli ya kompyuta (computer),Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ambayo inahusika katika maeneo yote ya Sayansi za kompyuta na kwamba wanatoa mafunzo ya mawasiliano ya habari kwenye maeneo tofauti tofauti.

"Katika skuli hii pia tuna programu ya habari 'Bachelor of mass communication' ambayo inafanya kazi ya kuwafundisha vijana wetu kuwa wanahabari bora ili waweze kuwa na uweledi na umakini lakini pia katika suala la maadili bora katika kazi zao wanazozifanya," ameaema Prof.Haji.


Prof. Haji ameongeza kuwa wanataasisi mbili ambazo zinafanya tafiti za kisayansi kwenye masuala ya bahari na mazingira yake katika ukanda wa 'tropical' na taasisi ambayo inasimamia lugha ya kiswahili ambayo pia inafanya tafiti mbalimbali katika kurahisisha matumizi bora na sahihi ya lugha hiyo pamoja na kukiingiza kiswahili katika soko la ulimwengu.

"Tunafahamu miongoni mwa tunu tulizonazo Tanzania  lugha ya kiswahili imekuwa ikifanya vizuri na ni bidhaa ambayo inahitajika ulimwengu kote, tumekuwa tukitoa msaada mkubwa kwa Vyuo mbalimbali duniani na taasisi nyingine kwa kupeleka Wataalamu tulionao wa lugha hii kwenda kufundisha na kutengeneza mitaala inayoweza kutumika huko na kuweza kufundisha wataalamu wao na hatimaye ongezeko la watumiaji  wa lugha hii liweze kukua mara dufu," ameeleza.

Amefafanua kwamba wanayafanya hayo kwa kuzingatia uwepo wa TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ambayo ina dhibiti shughuli zao zote na kwa kuwa chuo hicho kipo Tanzania taratibu za Uendashaji wa chuo kikuu zinaenda sawa na Vyuo vingine vilivyopo nchini.

Kwa mujibu wa Prof. Haji, SUZA ni miongoni mwa Vyuo 19 ambavyo vinashiriki katika utekelezaji wa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi kimsingi umelenga kutumia elimu hiyo na kuleta mageuzi hayo nchini kwa kuboresha miundombinu ya elimu na kutengeneza mitaala inayoakisi soko la ajira.

Pia amesema mitaala hiyo inalolenga kwenda kubadilisha na kuleta mageuzi ya kiuchumi, uingizaji wa matumizi ya TEHAMA kutokana na ulimwengu wa sasa umekuwa ukitumia TEHAMA hiyo katika mazingira yoyote.

"Kwa upande Tanzania mradi huu utaongeza nguvu kuhakikisha elimu ya juu inakwenda katika misingi ya matumizi ya TEHAMA iliyo sahihi ili kuleta maendeleo ya mageuzi ya kiuchumi, tunatoa pia nafasi za mafunzo ya walimu wetu katika vipaumbele vilivyoainishwa ili kuhakikisha mpango huu unasaidia Taifa kwa ujumla wake," amesema.

WANAOKOSA AJIRA SEKTA YA UMMA

Makamu huyo wa SUZA amebainisha kuwa wana eneo kubwa la vijana ambao wanakosa ajira katika sekta ya Umma wanapata nafasi ya kupata uwezo wa kujiajiri wenyewe kwa kutumia Stadi ambazo wanapatiwa za programu mbalimbali.

Amesema Chuo hicho kinafanya kazi ya kusaidia Umma kwa kuwapatia elimu na kuzisaidia serikali zote mbili ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutengeneza nguvu kazi iliyoimara yenye kuthubutu kufanya mageuzi na kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini.

"Tunaimarisha zaidi maadili ya kila mmoja, tunaamini maadili ni sehemu ambayo ina umuhimu katika kuleta ufanisi wa shughuli na kazi tunazozifanya kwa miaka 22 tuliyoifanyia kazi kama SUZA tumepata uzoefu mkubwa na tumeweza kujipanga katika maeneo ya mahitaji ya kimkakati, " ameeleza.

MAONESHO YA TCU

Akizungumzia maonesho yaliyoratibiwa na TCU Prof. Haji amesema wamepata fursa ya kuonana, kubadilisha mawazo na wadau mbalimbali wa elimu wakiwamo wanafunzi,watafiti, wanasayansi, sekta za viwanda pamoja na sekta nyingine za Umma na binafisi.

" Hii ni fursa iliyobora zaidi ya kukutana na kundi kubwa la wadau na kuwaonesha ni kitu gani sisi kwetu SUZA tunakitoa katika programu tulizonazo,tumepata fursa ya kupokea maoni mbalimbali na kipindi hiki vijana wetu wamemaliza masomo yao ya sekondari, kidato cha sita wanatumia muda huu kuangalia Vyuo vilivyobora ili kukidhi kiu zao za kupata elimu ya juu katika fani ambazo wanachagua," amebainisha.

Amesema chuo hicho kinazingatia misingi iliyobora kwa kuwapatia vilivyo vya ziada mbali na programu ambazo zipo nje ya mitaala lengo ni kuweza kuwawezesha vijana kutumia taaluma wanayoipata kwa kuongeza ujuzi na kutumia nafasi ya kubuni mbinu mbalimbali za kitaalamu za kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Prof. Haji ameongeza kwa mazingira yaliyopo soko la ajira limebebwa na sekta binafisi 
 na kwamba sekta za Umma zinajaribu kuchukua vijana wanaohitimu katika Vyuo vikuu lakini wengine wanabaki.

Profesa Haji ameongeza kuwa katika ngazi za kiutawala Baraza la Chuo hicho linafanya kazi kwa ukaribu ya kusaidia kwenye masuala ya uongozi ambayo wanayafanya chuoni hapo.

" Chuo hiki kimeanza mwaka 1999 kwa sheria iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi sheria namba 8 ya mwaka huo ambapo kilianza kazi rasmi za ufundishaji na utoaji wa elimu, tafiti pamoja na kazi nyingine mwaka 2021," ameeleza Prof. Haji.

Amesema tangu Chuo hicho kimeanza kimekuwa kikiongeza ubora wa kazi zake, pamoja na kujitanua katika maeneo mbalimbali huku akisema SUZA ilianza ikiwa na Taasisi moja ambayo inahusiana na masuala ya Sayansi za Elimu na Lugha.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI