WAKAZI SAME WAELIMISHWA ATHARI ZA MIRUNGI


 Na Mwandishi wetu 

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Wilaya Same imetoa elimu kwa wananchi wa kata ya Tae wilayani Same mkoani Kilimanaro kuhusu madhara ya kujihusisha na kilimo, biashara na matumizi ya dawa za kulevya aina ya mirungi ikiwa ni siku chache baada ya operesheni tokomeza mirungi iliyofanyika katika kata hiyo na kufanikisha 
uteketezai wa hekeri 535 za mashamba ya Mirungi na kukamatwa kwa watuhumiwa 9.

 Elimu hiyo imetolewa tarehe 11 Julai, 2023 katika kikao maalumu kilichowahusisha maafisa wa DCEA, viongozi wa wilaya ya Same, wataalamu ya masuala ya kilimo na bishara pamoja na wakazi wa kata hiyo. 

Akizungumzia athari za matumizi ya mirungi, Kamishna wa Kinga na Tiba DCEA, Dkt. Peter Mfisi ameeleza kuwa matumizi ya mirungi yanachochea uhalifu ikiwemo ugomvi na mauaji kwa sababu ya kuathiri uwezo wa kufikiri, jambo linalosababisha mtu kuchukua maamuzi yoyote pasipo kutafakari matokeo yake na kusema kuwa baadhi ya maeneo ambayo kilimo cha mirungi yamekithiri kuna changamoto kubwa wananchi wake kitabia.


“Watoto wenu wakianza kutafuna mirungi mtazalisha kizazi chenye migogoro na mafarano yasiyo isha. 

Watu mtashindwa kutatua hata changamoto dogo ndogo zinazowataka mkae chini na kuzijadili badala yake mnachukua mapanga na mikuki na kuanza kushambuliana” amesema Dkt. Mfisi.

Afisa kilimo wa halmashauri ya Same Bw. Mohammed Muhina ameyataja baadhi ya mazao ya biashara yanayostawi katika maeneo hayo yayoweza kuwa mbadala wa kilimo cha Mirungi.

“Eneo la Same linakubali mazao mbalimbali kama tangawizi, zao la vannila ambalo tayari limeanza kulimwa katika baadhi ya maeneo, lakini pia kuna zao la kahawa na mazao mengine mengi kama migomba na kadhalika” amesema Muhina.


Nae Kamishna wa Huduma za Kitengo cha Sheria DCEA, Veronica Matikila amesema Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Na. 5 ya Mwaka 2015 inakataza kilimo, kuhifadhi na ukusanya wa mazao haramu ikiwemo mirungi na bangi na adhabu yake ni kifungo cha miaka thelathini (30) jela au 
kifungo cha maisha. 

Hivyo, yoyote anayejishughulisha kwa namna yoyote na dawa za kulevya anatenda kosa na akibainika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo ametoa rai kwa viongozi wa halmashauri kuanzia maafisa tarafa na wenyeviti wa vitongoji kuwajibika
kuhakikisha wanadhibiti uhalifu wa kilimo na matumizi ya mirungi, pamoja na kutoa elimu kuhusu athari ya matumizi yake katika maeneo wanayosimamia kulingana na sheria za nchi.

"Ni wajibu wa kila kiongozi katika halmashauri kuhakikisha anadhibiti matumizi ya mirungi, ikiwa ni pamoja na kukomesha kilimo chake kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli mbadala wanazoweza kuzifanya ikiwemo kilimo cha mazao mengine yenye tija. Pia, kuwatumia wataalamu wa halmashauri kutoa ujuzi kwa wananchi utakaowasaidia kwa namna moja au nyingine kufanya biashara halali zitazokuwa chanzo cha mapato kwa ajili ya kujikimu na maisha na kuachana na biashara ya mirungi." amesisitiza Kamishna Jenarali Lyimo.


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni aliagiza viongozi wa kata ya Tae kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja visiki vyote ving’olewe na mashamba yote ambayo hayakufikiwa wakati wa operesheni yateketezwe, ambapo utekelezaji wake umeanza tarehe 12 Julai, 2023 ukiongozwa na afisa mtendani wa kata ya Likweni Isaack Stephano Mwansasu.

Vilevile, mkazi wa kata ya Tae, Elisante Semkondo amesema asilimia kubwa ya vijana katika kata hiyo wanatumia mirungi kutokana na tabia ya kuiga. Hivyo, ameishukuru Serikali kwa kuwapa elimu kuhusu mirungi na dawa za kulevya kwa ujumla kwa kuwa itaongeza hamasa kuchukua hatua ya kudhibiti
changamoto hiyo na kuachana kabisa na kilimo cha mirungi.

Operesheni hiyo ya kutekeza mirungi katika mkoa wa Kilimanjaro ni hatua ya Serikali katika kuhakikisha inadhibiti na kutokomeza matumizi ya dawa ya kulevya na imekuja ikiwa wiki kadhaa tangu kufanyika Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya mkoani Arusha ambapo mgeni rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan aliagiza kufanyika kwa operesheni endelevu ikiwa ni pamoja na viongozi wote wa Serikali kushiriki katika kupambana na dawa za kulevya katika maeneo yao.

Katika kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais, Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda akishirikiana na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya jana tarehe 13 JulaI, 2023 ameviongoza Vyombo vya Ulinzi na Usalama wilayani humo katika operesheni maalumu katika kijiji cha Kisimiri na kufanikiwa kuteketeza gunia 280 na mbegu kilogramu 300 za bangi na kukamatwa kwa watuhumiwa 4 wakihusishwa na bangi hizo.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU