BMH IMELENGA KUONDOA TATIZO LA 'SICKLE CELL', WAZAZI WASHAURIWA

Mtaalam wa upimaji wa uono na miwani kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH),Godfrey Felix, akimpima mteja aliyetembelea banda la hospitali hiyo katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Na Asha Mwakyonde, Mbeya

WAZAZI wenye watoto ambao wana tatizo la ugonjwa wa Selimundu (sickle cell), wameshauriwa kufika katika vituo vya afya ili kupata taarifa sahihi ikiwa ni pamoja na kwenda katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH),kupata maelezo sahihi na kufanya upimaji wa ugonjwa huo.

Akizungumza jijini Mbeya leo 2, 2023, katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu kutoka Hospitali hiyo, Dk. Stella Malangahe amesema kuwa hospitali ya Benjamin Mkapa imeanzisha huduma mpya ya upandikizaji wa Uloto ili kuondoa matatizo ya Selimundu endapo mtoto atakuwa amezaliwa na ugonjwa huo.

Dk.Malangahe amesema huduma hiyo ni mpya katika hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo imeanzishwa Januari mwaka huu na hadi sasa wamepandikiza Uloto kwa watoto wanne waliokuwa natatizo la Selimundu.

"Huduma hii imefanikisha kuondoa tatizo hilo kwa watoto waliokuwa na tatizo la Selimundu, tunafahamu kwamba Selimundu ni ugonjwa wa kurithi ambao mtoto anaupata kutoka kwa wazazi wake baba na mama kwa kurithi vinasaba vibovu na kwenda kutengeneza chembe chembe za damu nyekundu ambayo inakuwa na hitilafu inayoshindwa kufanya kazi vizuri ya kusafirisha damu," amesema.

Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa huduma hiyo Tanzania imekuwa nchi ya sita katika nchi ambazo zinatoa huduma ya kupandikiza Uloto na ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

Daktari huyo ameeleza kuwa wapo katika maonyesho hayo kwa ajili ya kutoa taarifa sahihi kwa jamii na wakifika watapata taarifa zote sahihi zinazohusiana na upandikizaji wa Uloto na nyingine zinazohusiana na magonjwa ya damu.

"Huduma ambayo tunaitoa katika hospitali hii ni pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje wenye matatizo ya upungufu wa damu kushindwa kufanya kazi vizuri lakini pia tuna kiliniki maalumu kwa ajili ya watu wenye matatizo ya Selimundu pamoja na saratani za damu," amesema daktari huyo.

Awali Ofisa Uhusiano kutoka Hospitali hiyo Raymond Mtani amesema kuwa wapo Katika katika maonesho hayo ambapo wamepeleka huduma mbalimbali na kuwapatia  wananchi elimu kuhusu huduma za matibabu ya ubingwa bobezi ambazo zilikuwa hazipatikani   nchini na wagonjwa walikuwa wakienda kutibiwa nje ya nchi.

Amesema kuwa wapo madaktari bingwa wa magonjwa ya upandikizaji wa figo kwa ajili ya kuzungumza na watu wanaotembelea banda hilo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na afya ya figo.

"Tupo na  daktari bingwa wa upandikizaji wa Uloto kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa selimundu, daktari wa kuzibua masikio na pua pamoja na daktari bingwa wa magonjwa ya macho ambaye anatoa huduma ya kupima macho na huduma hizi ni bure katika banda letu," amesema.

Ameongeza kuwa  katika banda hilo la Hospitali ya Benjamin Mkapa inatoa huduma za dharura kwa watakaougua wakiwa kwenye maonesho hayo.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI