Na Asha mwakyonde,Mbeya
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amekipongeza Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),kwa ubunifu mashine zinazowasaidia wakulima na wafugaji kuzalisha chakula kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.
Akizungumza Jumatano Agosti 2, 2023 kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', alipotembelea banda la NIT amesema amefurahishwa na Chuo hicho kwa kupiga hatua.
Naibu Waziri huyo ameelezakuwa miaka ya 2005 kurudi nyuma chuo hicho hakikuwa kama kilivyo Sasa ambapo kilikuwa na wanafunzi wachache wasiosidi 500.
"Kwa sasa Chuo hiki kina wanafunzi zaidi ya 12,000 ambao wanapata mafunzo na kozi mbalimbali ambazo ni za kimkakati za kulisaidia Taifa katika Miradi yake mikubwa.
Nao wanafuanzi Wahandisi wa Mitambo kutoka Chuo hicho wamebuni mashine zinazowasaidia wakulima na wafugaji kuzalisha chakula kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.
Mhandisi wa Mitambo Hytham Kalenge amebuni mashine ya kusaga nafaka ambayo inamrahisishia mjasiriamali amesema mashine hiyo inatumia umeme na ukikatika itaendelea kufanya kazi.
Ameongeza kuwa lengo la kubuni mashine hiyo ni kumuondolea changamoto mjasiriamali na kumrahisishia kuzalisha bidhaa zake kwa muda mchache.
"Mashine hii inawezesha wajasiriamali wa kati kuzalisha chakula kwa wingi ambapo inasaga nafaka na kuchanganya kilo 20 kwa saa hii itasaidia pia kuzalisha bidhaa nyingi na kwa wakati," ameeleza.
Naye Adventina Stambuli amesema mashine aliyobuni inawezesha wafugaji wadogo kuzalisha chakula kingi cha mifugo kwani inachakata kilo 100 kwa saa na kumpunguzia gharama za kuzalisha na muda.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa chuo hicho,Juma Mandai, amesema wanafunzi hao kabla ya kumaliza masomo yao wanafanya projekti
za kibunifu ili wanapomaliza waweze kuwa msaada katika jamii.
“Tupo hapa kwenye maonesho haya kuonyesha mashine hizi kwa wadau ili kuleta hamasa ya vijana kujiunga na chuo na kuweza kupata ujuzi ambao itawasaidia wao na jamii kwa ujumla,"ameeleza.
0 Comments