Na Asha Mwakyonde, Mbeya
CHAMA Kikuu cha ushirika cha Kagera (KCU),kimetenga zaidi ya Sh milioni 950 kwa ajili ya kuanzisha vyama vya kuweka akiba na mikopo (SACCOS), itakayowasaidia wakulima kuondokana kuuza kahawa kwa bei zisizo rasmi.
Akizingumza jijini Mbeya leo Agosti 4, 2023, Mwenyekiti wa Bodi ya KCU Ressy Mashulano kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', wakati akitoa maelezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa,Gerald Kusaya alipotembelea banda chama hicho.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa SACCOS hiyo ipo katika hatua za mwanzo na wanatarajia ifikapo mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka huu watakuwa tayari wameshaianzisha
Ameongeza kuwa chama hicho kinaundwa na vyama vya msingi 142 na kina wamachama 70,000 ambao wanazalisha kawaha aina ya robusta kwa asilimia 97 na asilimia 3 ni aina ya Arabica ngumu na kwamba wanamiradi ukiwamo wa mashamba hivyo wanaendesha shughuli zao kwa faida kubwa.
Amesema Mkoa wa Kagera ndio unaozalisha kahawa kwazaidi ya asilimia 55 nchini na kwa sasa wakulima wa zao hilo wanafuraha ambapo chama hicho kinaendesha minada ya moja kwa moja.
Ameongeza kuwa msimu uliopita wameweza kurudisha faida kwa wakulima ya Sh. Milioni 6,410,000
Naye Meneja Mauzo nje ya nchi wa KCU Josephat Sylvand amesema awali ilikuwa ni Sh. 1100 hadi 1500 kwa tani ambapo kwa sasa ni 2500 hadi 2600 na muda mwingine 2800 hasa kahawa aina ya Arabica.
"Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita ikilinganishwa na mika 15 ya nyuma bei iliyofikiwa kwa sasa haijawahi kutokea," amesema.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa Kusaya amekipongeza chama hicho kwa hatua nzuri za mafanikio kwa wakulima yakiwamo ya kutaka kuanzisha SACCOS.
0 Comments