Na Asha Mwakyonde,Dodoma
JUMLA ya ajira 145,245 zimezalishwa kwa Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati ya uwekezaji
ambapo wanawake ni 29,049 sawa na 20 na wanaume 116,196 sawa na asilimia 80 hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma leo Agosti 14, 2023 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Being'i Issa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya Baraza hilo kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024, amesema jumla ya kampuni za Kitanzania 2, 010 zimenufaika kwa kupata kazi mbalimbali katika miradi inayosimamiwa na kuratibiwa na NEEC.
Ameeleza kuwa ongezeko la ushiriki wa Watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji (Local Content),Baraza linaratibu masuala ya Local Content katika sekta za kipaumbele ambazo ni mafuta na gesi, kilimo, ujenzi, viwanda, utalii na sekta mtambuka.
Katibu huyo akizungumzia mafanikio ya Baraza hilo katika mifuko ya uwezeshaji amesema hadi kufikia Machi, 2023 mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 6.1 ilitolewa kwa wajasiriamali 8,650,257 ikiwa wanawake ni 4,747,321 na wanaume 3,902,936.
Amesema lengo ni kutoa fursa kwa Watanzania kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati, kupata mikopo yenye riba nafuu hususan kwa viwanda vinavyochakata mazao ya kilimo na mifugo.
"Mafanikio katika kuendeleza viwanda vidogo na kati (SANVN Viwanda Scheme), hadi kufikia Juni 2023 mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.8 ilitolewa kwa miradi 65 katika mikoa 13," amesema.
Akizungumzia baadhi ya vipaumbele vya Baraza hilo kwa mwaka 2023/2024, amesema
ni kukarabati vituo vya Uwezeshaji katika Halmashauri ambazo ni Halmashauri ya Nyang’wale, Mlele na Mbinga, kuingia makubaliano na Chama cha Wakandarasi Tanzania ili kuboresha shughuli za ujenzi kwa walengwa wa miradi ya ujenzi hapa nchini.
" Pia tutaingia makubaliano na shirika la misaada la Marekani USAID katika kuboresha maeneo mbalimbali ya wafanyabiashara hapa nchini," amesema.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa ,Idara ya Habari MAELEZO Gerson Msigwa amewataka Watanzania kuwa makini na kujiridhisha kabla ya kuingia mikataba ya kuchukua mikopo ili kuepuka madhara yanayotokana na mikopo hiyo kutoka kwa taasisi zisizo rasmi.
"Mikopo yote inapitia kwenye ngazi za Halmashauri, fuateni taratibu zote ili kuepuka kutapeliwa hasa mikopo inayotangazwa mitandaoni," ameeleza.
Majukumu ya Baraza hilo ni kusimamia, kuratibu, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi Tanzania Bara.
0 Comments