Na Asha Mwakyonde,Dodoma
TAASISI ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (Tanzania Official Seed Certification Institute (TOSCI), katika mwaka wa Fedha 2023/2024 imetengewa kiasi cha Shilingi bilioni 12.6 kwa ajili ya utekelezaji majukumu yake ambayo ni vipaumbele vya taasisi hiyo.
TOSCI ni Taasisi ya serikali iliyopo chini ya Wizara ya Kilimo iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mbegu Namba 18, ya mwaka 2003 ikiwa na jukumu la Kuthibitisha na kukuza mbegu bora za kilimo zinazozalishwa, zinazoingizwa nchini kwa ajili ya kuuzwa na kulinda jamii ya wakulima dhidi ya mbegu duni (feki) kutoka kwa wauzaji wa pembejeo za kilimo.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma leo Agosti 15,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI Patrick Ngwediagi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024 amesema lengo la serikali kutenga fedha hizo ni kwa ajili ya kuendelea na uboreshaji wa shughuli za usimamizi wa ubora wa mbegu.
Akizungumzia vipaumbele vingine vya taasisi hiyo amesema kutekeleza mradi wa kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi (AFDP), kwa kuboresha shughuli za uthibiti na usimamizi wa ubora na uthibiti kwa kujenga maabara ya kuchambua mbequ makao makuu Morogoro,kujenga na kufanya ukarabati wa maabara ya mbegu Kanda ya Ziwa Mwanza.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa vipaumbele vingine ni pamoja na kuandaa na kutekeleza mkakati wa kuelimisha umma juu ya matumizi ya mbegu zilizothibitishwa ubora na zenye lebo ya TOSCI, kuthibitisha na kusimamia ubora wa miche, vipando na pingili za mazao ya miti ya matunda, migomba na miwa.
Akizungumzia mafanikio ya taasisi hiyo amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 TOSCI ilitengewa kiasi cha Shilingi bilioni 10.6 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi kwa ujumla.
"Taasisi ilitoa mafunzo kwa wafanyabiashara ya mbegu 1,832 na kusajili aina 1,031za mbegu, kufanya majaribio ya utambuzi wa mbegu aina 49 na umahiri wa aina mpya za mbegu 18 na usajili na ukaguzi wa mashamba ya mbegu 1,554," ameeleza Ngwediagi.
Ameeleza kuwa mafanikio mengine ni uchukuaji wa sampuli 54,000 za mbegu kwa ajili ya vipimo vya maabara, utoaji wa lebo za TOSCI 12,354,358, ukaguzi wa maghala ya kuhifadhia mbegu 180 na maduka ya mbegu 4,500.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo utoaji wa vibali vya kuingiza mbegu nchini kutoka nje 27,503, kuuza nje 23, na aina za mbegu 1,172 ziliuzwa nje ya nchi na utoaji wa mafunzo ya kuimarisha taaluma za watumishi 45 wa TOSCI.
0 Comments