WAKALA WA VIPIMO: WANYAMA KUUZWA KULINGANA NA UZITO

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA), imesema kuwa imehakiki Mizani 84 iliyonunuliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), kwa ajili ya kusambazwa kwenye minada mbali mbali ya mauzo ya Wanyama lengo likiwa ni  kuhakikisha Wanyama wanauzwa kulingana na uzito na sio kwa muonekano wake.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma leo Agosti 15,2023 na Afisa Mtendaji wa WMA Stella Kahwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji  wa majuku na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/ 2024 wa Wakala huo.

Amesema kuwa katika kufanikisha lengo hilo, mwezi Februari, 2023, 
Wakala wa Vipimo imeendelea kuhakiki Mizani inayotumika kwenye minada ya kuuzia Wanyama.

Afisa huyo  amesema ili kuendeleza kutoa mchango kwenye sekta ufugaji  Wakala imeendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi katika kufanya malisho ya Wanyama, uuzaji wa Wanyama kwa uzito pamoja malighafi kama mbolea.

"Sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi kutokana na umuhimu huu ni dhahiri kuwa ipo haja ya kuendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa na kuchakata,kusarifu bidhaa za mifugo kwa ajili ya mahitaji ya ndani, ikiwemo ya lishe bora, na usafirishaji nje," ameeleza.

Akizungumzia sekta ya kilimo amesema katika kuhakikisha kilimo kinaendelea kuwa nguzo muhimu kwa  kuchochea uchumi wa nchi, Wakala wa Vipimo imeendelea kufanya uhakiki wa vipimo vinavyotumika kwenye kilimo  hicho ambavyo kwa sehemu kubwa ni mizani. 

"Kwa mfano katika mazao ya kimkakati katika kipindi cha mwaka 2022/2023 wakala ilihakiki jumla ya mizani 4254 ambapo Pamba ni 1566, Korosho 2286 na Kahawa 402," amesema. 


Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO Gerson Msigwa amesema kuwa  Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amepeleka fedha nyingi katika sekta hiyo ili kilimo kiwe cha kitaalamu.

"Wananchi wanatakiwa kutoa taarifa zinazohusu masuala ya rumbesa ili serikali iwachukulie hatua kwa wanaofanya vitendo hivi vya rumbesa," amesema Msigwa.

Aidha amewataka waandishi wa habari kuandika mara kwa mara  habari zinazohusu masuala ya rumbesa ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika kufichua wafanyabiashara wanao wasababishia wakulima hasara.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI