TFS YAPANDISHA HADHI MISITU 15 KUWA YA KITAIFA

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

WAKALA wa Misitu Tanzania( TFS ) umefanikiwa kupandisha hadhi Misitu ya hifadhi 15 kuwa Misitu ya hifadhi ya Taifa na Misitu ya hifadhi za mazingira asilia mitano 5 yenye ukubwa wa hekta 58,216 katika kipindi Cha Mwaka 2022/2023 ambapo Upandishaji hadhi huo,utafanya Misitu hiyo kutumiwa kwa shughuli za utalii na uwekezaji

Kamishna wa uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Profesa. Dos Santos Silayo, ameyasema hayo Leo Jijini Dodoma,wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala huo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Profesa Dos Santos, ameitaja Misitu hiyo kuwa ni; Kindoroko (Mwanga), Nou (Mbulu/Babati), Uvinza (Uvinza), East Matogoro (Songea) na Hassama Hill (Mbulu). 

Kamishna huyo ameeleza kuwa kufuatia juhudi za serikali ikiwemo ubunifu wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuandaa filamu ya “Tanzania the Royal Tour” ambayo imeitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi kwa kiasi kikubwa, TFS imejipanga kutumia fursa hiyo kuongeza tija katika uhifadhi, utalii na ukusanyaji maduhuli.

 "Juhudi hizo zimesaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea vivutio vya utalii ikolojia ambapo hadi kufikia Juni 2023 jumla ya watalii 242,824 walitembelea vivutio hivyo,"ameongeza.


“Idadi hii ni ongezeko la asilimia 60.8 ukilinganisha na watalii 152,002 waliotembelea vivutio hivyo kwa kipindi hicho kwa mwaka 2021. Jumla ya sh.bilioni 1.3 zilikusanywa ikilinganishwa na sh.milioni 603.3 zilizokusanywa mwaka uliopita ikiwa ni ongezeko la Asilimia 126.9,"ameeleza.

Amebainisha kuwa :”Katika kipindi cha miaka miwili TFS tumeanzisha shamba jipya moja la Makere Kasulu-Kigoma, na kufanya upanuzi wa mashamba mawili,

Katika hatua nyingine, profesa Silayo amesema katika mwaka wa fedha uliopita, TFS ilizalisha jumla ya tani 25.9 za mbegu za miti na kuotesha miche milioni 32.7 ya aina mbalimbali ambayo ilipandwa katika mashamba 24 ya serikali na mingine kugawiwa kwa watu binafsi, taasisi na mashirika mbalimbali kwa ajili ya kupandwa katika maeneo yao.

Amesema kuwa hadi sasa, TFS imepanda miti katika hekta 6,909 na kurudishia miti iliyokufa kwenye hekta 2,434 pamoja na kuendeleza mashamba ya miti kwa kupalilia hekta 31,197, kupogolea hekta 8,353 na kupunguzia miti kwenye hekta 2,785.

”Wakala umeandaa mkakati wa usimamizi na uendelezaji wa mashamba ya miti ya serikali wa miaka 30 kuanzia 2021 hadi 2050 ambao umelenga kupanua wigo wa aina ya miti ya ikiwemo ile ya madawa kama vile Prunus africana na mpira .Miti hii imeanza kupandwa katika mashamba ya Mbizi, Wino, Rongai, Saohill, Iyondo Mswima, Meru na Shume,”alieleza

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI