Na Asha Mwakyonde,Dodoma
ZAO la mkonge limeongeza uzalishaji kutoka tani 36,379 kwa mwaka 2020 hadi kufikia tani 48,351.49 mwaka 2022 na kuongezeka kwa fedha za maendeleo kutoka shilingi milioni 100 mwaka 2019/2020 hadi kufikia shilingi bilioni 2 mwaka 2022/2023.
Akizungumza jijini Dodoma leo Agosti 16,2023 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saad Kambona, kuhusu utekelezaji na mwelekeo wa taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024,ameeleza kuanzia mwaka 2018, Serikali iliamua kuchukua hatua za makusudi za kufufua zao la Mkonge na kuifufua na kuijenga upya Bodi hiyo.
Mkurugenzi huyo amesema mwaka 2019, Serikali lifanya mageuzi ya kuliingiza zao hilo katika orodha ya mazao ya kimkakati na kulifanya kuwa zao la saba la kimkakati.
Ameongeza kuwa zao la Mkonge likaingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 hadi 2025 na kuwekewa lengo la kuongeza uzalishaji kutoka tani 36,000 zilizokuwa zinazalishwa kwa mwaka 2020 hadi kufikia tani 80,000 kwa mwaka ifikapo Mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Serikali iliongeza lengo na kuiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 kwa mwaka, ifikapo mwaka 2025/2026.
Amebainisha kuwa mageuzi hayo yamesababisha kuongezeka kwa fedha za makusanyo ya ndani kutoka shilingi 0.00 mwaka 2019/2020 hadi shilingi milioni 507 mwaka 2022/2023 na kuweza kukusanya na kusambaza miche 6,991,200 ya mbegu za Mkonge bure kwa wakulima wadogo katika Wilaya 16 kumechangia.
"Mwaka 2020, TSB iliweza kusajili wakulima wadogo 6,887 mwaka 2022, idadi ya wakulima wadogo waliosajiliwa ni 8,972. Hata hivyo, wakulima wadogo wa Mkonge ambao hawajafikiwa na kusajiliwa na TSB wanakadiriwa kufikia 22,000," ameeleza.
Aidha amesema kuwa Bodi hiyo imegawa mashamba kwa wakulima 983 wilayani Korogwe na wakulima wengine zaidi ya 3,000 wamegawiwa mashamba wilayani Kilosa na zoezi bado linaendelea.
0 Comments