REA KUSAMBAZA MAJIKO 200,000 VIJIJINI NA VIJIJI MIJI


Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

WAKALA  wa Nishati Vijijini (REA), umeanza kutekeleza mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia (LPG),71,000 yenye thamani ya shilingi bilioni 3 pamoja na majiko banifu 200,000 katika maeneo ya vijijini kwa utaratibu wa utoaji ruzuku.

Pia Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), imetenga Dola za Marekani milioni 6 kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa majiko banifu ya kupikia ambapo takribani majiko 200,000 yanatarajiwa kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya vijijini na vijiji miji Tanzania bara. 

Akizungumza jijini Dodoma leo Agosti 18,2023 Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy kuhusu utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa Wakala huo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 amesema  jumla ya fedha takribani shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha mradi huo.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa mradi wa Kusambaza Gesi Asilia (CNG) unahusika na kusambaza gesi asilia ya kupikia katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.

Ameongeza kuwa utekelezaji wake utahusisha REA na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)  ambapo kwa mwaka wa Fedha 2023/24, jumla ya shilingi bilioni 20 zinatarajiwa kutumika.

"Mradi huu utahusisha ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia (CNG) lenye urefu wa KM 44.4 (Mnazi Mmoja – Lindi (km 22.9) na Mkuranga – Pwani (KM 21.5)) na jumla ya nyumba/wateja 980 kunufaisha (Mnazi Mmoja – Lindi, wateja 451 na Mkuranga-Pwani, wateja 529)," ameeleza Saidy.

Akizungumzia usambazaji wa majiko hayo Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa wanufaika wa mradi huo ni wazalishaiji na wasambazaji wadogo wa ndani wa majiko banifu. 

"Lengo la mradi huu ni kukuza na kuboresha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ambapo kwa sasa, Wakala upo kwenye mchakato wa uandaaji wa taratibu na kanuni za utoaji wa ruzuku hizo," amesema.

Akizungumzia mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili unahusisha kupeleka umeme kwenye vijiji 4,071 vilivyobaki kati ya vijiji vyote 12,318 pamoja na kujenga njia za umeme wa Msongo wa Kati zenye urefu wa kilomita 23,526, kujenga njia za umeme wa Msongo Mdogo zenye urefu wa kilomita 12,159, kufunga mashineumba 4,071 na kuunganisha wateja wa awali wapatao 258,660. 

Amefafanua kuwa mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kwa kiasi cha shilingi trilioni 1.58. 

"Mradi huu kwa sasa upo katika hatua ya utekelezaji ambapo unatarajiwa kukamilika Disemba 2023 kwa mikataba 32 na Juni 2024 kwa mikataba saba (7). Utekelezaji wa mradi kwa sasa umefikia wastani wa asilimia 73. 

Kwa upande wake  Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Gerson Msigwa amesema mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kupitia Bwawa la Nyerere, umefikia zaidi ya asilimia 90 huku akisema  ifikapo mwezi Juni umeme unaanza kupelekwa kwenye Gridi ya Taifa.

"Pamoja na jitihada za kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote nchini vinapata umeme, Serikali inayo mambo mengine ambayo lazima yafanyike ili REA iweze kufanya kazi yake vizuri ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme," ameeleza.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA