TUME YA MADINI YATOA LESENI 9,642 KATI YA 9,174 ZA UCHIMBAJI


Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

KATIKA mwaka wa fedha 2022/23, Tume ya Madini ilifanikiwa kutoa jumla ya leseni 9,642 kati ya leseni 9,174 zilizopangwa kutolewa ikiwa ni kuimarisha uwekezaji katika sekta ya hiyo nchini.

Pia Tume hiyo imesema kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanikiwa kuanzisha jumla ya masoko ya madini 42 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 94 nchini.

Hayo yameelezwa leo Agosti 18 jijini Dodoma na Kaimu katibu Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo Ramadhan Rwamo wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha mwaka 2022/23 na mikakati ya mwaka 2023/24.

Ameeleza kuwa leseni hizo zilijumuisha leseni za uchimbaji mkubwa, uchimbaji wa kati, uchimbaji mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini,

Mtendaji huyo amesema kati ya leseni zilizotolewa leseni 6,511 sawa na asilimia 70.97 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo,hiyo inadhihirisha azma ya serikali ya awamu ya 6 katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika sekta ya madini.

"Muelekeo wa sekta ya madini unalenga katika kuhakikisha mchango wa sekta ya hii katika Pato la Taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama inavyofafanuliwa katika dira ya maendeleo ya Taifa,ilani ya chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na Mpango mkakati wa Tume ya madini wa mwaka 2019/20-2023/24," amesema 

Akizungumzia uanzishwaji wa masoko hayo  Mtendaji huyo amesema ulianza rasmi tarehe 17 March 2019 kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa biashara ya madini nchini ili kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini kwa Serikali.

Rwamo amefafanua mwaka wa fedha 2022/2023 masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilichangia jumla ya shilingi 157,428,350.41 kama mrahaba na ada ya ukaguzi wa madini nchini sawa na asilimia 23.22 ya makusanyo yote yaliyokusanywa na Tume kwa mwaka husika.

Tume ya Madini ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya madini ambayo iliundwa na sheria ya madini sura ya 123 na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Na.27,na ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi tarehe 17 aprili 2018.

Lengo kuu la kuundwa kwa Tume ni kuboresha usimamizi na Udhibiti katika ukaguzi wa uzalishaji na biashara ya madini kwa kuhakikisha sheria,kanuni na taratibu zote zinazoongoza shughuli za madini zinafuatwa ipasavyo ili kuongeza pato la Taifa.

Majukumu ya Tume ya madini yamefafanuliwa katika sheria ya madini sura ya 123 kifungu cha 22 ambayo yanalenga kusimamia shughuli zote zinazohusiana na madini nchini.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA