SERIKALI YAANDAA MFUMO WA RUFAA KWA WAHAMIAJI WALIOKO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI HUSUSANI WATOTO


Kamishna wa Ustawi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuuandaa Mfumo wa Rufaa kwa wahamiaji walioko katika mazingira hatarishi hasa watoto, kilichofanyika Agosti 22, 2023 jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la uhamiaji (IOM) Ken Heriel akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuandaa mfumo wa rufaa kwa wahamiaji walioko katika mazingira hatarishi hasa watoto kilichofanyika Agosti 22, 2023 jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Watoto (UNICEF) Mbelwa Galagambi akizungumza wakati wa Kikao kazi ya kuuandaa Mfumo wa Rufaa kwa wahamiaji walioko katika mazingira hatarishi hasa watoto kilichofanyika Agosti 22, 2023 jijini Dodoma.

Kamishna wa Ustawi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha kuuandaa Mfumo wa Rufaa kwa wahamiaji walioko katika mazingira hatarishi hasa watoto kilichofanyika Agosti 22, 2023 jijini Dodoma.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,WMJJWM

Na Witness Masalu WMJJWM, Dodoma

WIZARA ya Maendeleo  ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali  inaandaa mfumo wa Rufaa kwa wahamiaji walioko katika mazingira hatarishi hususani watoto ikiwa ni Juhudi ya kuhakikisha ustawi  na Mazingira salama ya Watoto nchini.

Akizungumza katika Kikao kazi hicho, Kamishna wa Ustawi Nchini, Dkt Nandera Mhando amesema maandalizi ya Mfumo huo unashirikisha watu kutoka ngazi za chini Kitaifa ili kuweza kupata taarifa sahihi za hali ya Wahamiaji walio katika mazingira hatarishi hususani watoto ili kuja na suluhu sahihi.

“Mfumo wa taarifa sahihi kwa wakati utapunguza madhara au kuyaondoa kabisa na uundaaji wa Mfumo huu wa rufaa unalenga kufanya hivyo. Katika kuandaa mfumo huu tunatakiwa kuhakikisha kwamba unaweza kutumika ndani na nje ya nchi kwani usafirishaji wa watoto kwenda kufanya kazi katika mazingira magumu bado ni changamoto “ alisema Dkt. Nandera.

Aidha Dkt. Nandera amesema Ili mfumo huo uweze kuwa na manufaa zaidi itabidi uweze kuwa na taarifa za makundi mengine yote ambayo yapo katika hatihati  ya kukatiliwa ,yaani kuwa na mfumo jumuishi  ili kundi la wahamiaji hususani watoto walio katika mazingira hatarishi kuwa ni tawi kwenye Mfumo  huo jumuishi nchini.

Naye, Mwakilishi kutoka shirika la kimataifa la Uhamiaji(IOM),Ken Heriel amesema kikao kazi hicho kimeshirikisha wadau mbalimbali kutoka mikoa mitatu ya Tanzania ambayo ni Kigoma, Mbeya na Dar Es Salaam ambapo mikoa hiyo ni kati ya mikoa iliyoko kwenye hatari zaidi ya wahamiaji hususani watoto walioko kwenye mazingira hatarishi.

“Mfumo huu umelenga kupata namna sahihi ya upatikanaji wa taarifa yaani kuweza  kuwafuatilia kwa ukaribu zaidi hata pale watoto wanaporudishwa kwenye Nchi zao inakuwa rahisi kuwa na Taarifa zao sahihi  ili kuhakikisha watoto wanakuwa salama “alisema Heriel.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la Watoto, Mbelwa Gabagambi amesema katika uandaaji wa  mfumo huo wa Rufaa utawezesha marekebisho ya vipengele ikiwemo sheria na Kanuni zinazohitaji marekebisho.

“Sheria na Kanuni tayari zipo,lakini kupitia uundaji wa mfumo huu itakuwa rahisi kwa serikali kujua ni wapi pana changamoto na  kupelekea marekebisho ikiwa ni jitihada za kulinda maslahi na ustwai wa mtoto” alisema Gabagambi

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU