TANZANIA NA MALAWI ZAKUBALIANA KUZALISHA UMEME WA MAPOROMOKO

Na Asha Mwakyonde, Dar es salaam

WAZIRI wa Nishati, January Makamba, amesema serikali ya Tanzania na Malawi zimekubaliana kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya Maji ya Mto Songwe pamoja na kuendeleza rasilimali za mto huo ikiwa ni maelekezo ya Marais wa nchi hizo, Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Lazarus Chakwera walipokutana hivi karibuni.

Marais wa nchi hizo hivi karibuni 
walikubaliana kuendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali yakiwamo kudumisha uhusiano uliopo.


Akizungumza Agosti 11, 2023 wakati wa kusaini makubaliano hayo Dar es Salaam, Waziri Makamba ameeleza kuwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga njia ya kusafirisha umeme itakayounganisha nchi hizo tayari umekamilika ambapo kwa sasa wanatafuta fedha mradi uanze kutekelezwa.

Amesema wanatarajia kuzalisha umeme wa megawati 180 kwa kutumia maporomoko ya Mto Songwe na kwamba makubaliano hayo yatahusisha ujenzi wa miundombinu ya umeme na katika eneo la gesi ambapo Tanzania inatarajia kuuza gesi Malawi.

Waziri huyo amesema hiyo ni sehemu ya mradi wa kikanda wa kuwa na gridi moja katika kanda hii.

Waziri huyo ameongeza kuwa  maelekezo ya viongozi  hao walikubaliana waongeze maeneo ya ushirikiano hasa katika  eneo la nishati.

"Kila upande utateua wataalam na vikao vitaanza rasmi Oktoba mwaka huu na kamati ya pamoja ya mawaziri na kamati ya wataalam," ameeleza Waziri Makamba.

Kwa mujibu wa Waziri Makamba, kamati ya wataalam itaamua eneo sahihi la mradi kutokana na taarifa za kiufundi zitakazopatikana.

Amesema kuwa waaamini miradi hiyo  itanufaisha nchi  hizo kwa kuwa  mahitaji ya umeme bado ni makubwa na ushirikiano huo utaimarisha uhusiano kati ya nchi za Tanzania na Malawi.


Naye Waziri wa Nishati Malawi, Ibrahim Matola, amesema makubaliano hayo yataleta manufaa kwa nchi zote mbili huku akisema makubaliano hayo ni mwanzo wa safari yao ya kushirikiana katika nyanja nyingine. 

Amesema nchi nyingi Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki bado hazina nishati ya kutosha hivyo ni muhimu kuwe na miradi mingi zaidi katika sekta hiyo.

Post a Comment

0 Comments

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA