TCDC YAJA NA MFUMO WA MUVU NANE NANE, WASIOUTUMIA KUONDOLEWA


Na Asha Mwakyonde,Mbeya

TUME  ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania ( TCDC), imeanzisha Mfumo wa Usimamizi wa vyama vya ushirika (MUVU), lengo likiwa ni kuvirahisishia vyama vya ushirika katika utendaji wake pamoja na kuvipunguzia gharama na muda wa kwenda kwenye ofisi za Mrajis Mkoa au Taifa.

TCDC imesema viongozi ambao bado wanapiga piga chenga kutumia mfumo huo tume hiyo ina mamlaka ya kuwaondoa kwenye nafasi zao na kuruhusu chama kupata viongozi wengine.

Akizingumza jijini Mbeya leo  Agosti 6, 2023, katika banda la TCDC, Mrajis wa Vyama Vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo Ushirika Tanzania (TCDC) Dk. Benson Ndiege kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', amesema Tume hiyo ndio msimamizi wa vyama vya ushirika nchini kwa mujibu wa sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013.

Mrajis huyo amesema kuwapo kwa mfumo huo kutakuwa na mwanya mdogo na watu wachache kutumia ile mifumo ambayo sio ya wazi kuweza kuwaibia wanaushirika.

"Tume ya maendeleo ya Ushirika ni moja ya washiriki katika maonesho haya, eneo hili tulilopo wanaliita kijiji cha ushirika, kwa maana kuna serikali, wanaushirika wenyewe wote wamekusanyika hapa kwa pamoja na wanapokuwa hapa wanajifunza namna ya kuongeza uzalishaji," amesema.

Mrajis huyo ameeleza kuwa katika maonesho hayo TCDC imeleta MUVU, na kwamba siku za nyuma walikuwa na changamoto kubwa ya Usimamizi wa vyama hivyo.

"Kama serikali tumeamua kuja na mfumo wa Usimamizi wa vyama vya ushirika ambao utasimamia shughuli zote za vyama hivi,  wanapoomba bajeti zao,kufanya mikutano mikuu, wanapo ajiri na mambo mengine yote yatakuwa yanaonekana kwenye mfumo utasaidia kukiangalia chama  kwa ukaribu zaidi," ameongeza.

"Mfumo huu sio lazima nifike kwenye chama ndio nijue taarifa ya mwanacha  naweza kuangalia taarifa zake za mwezi kwenye mfumo,"ameeleza.

Ameongeza kuwa kuna banda la benki ya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KCBL), ambayo imebaki moja hapa nchini na wanaushirika wapo kwenye mpango wa kuibadilisha kuwa benki ya Taifa ya Ushirika.

Amesema  hayo ni mambo mawili ambayo wameyapeleka katika maonesho mfumo pamoja na benki hiyo ambayo wameyapeleka kuonesha na kuwahamasisha wadau wengine kuweza kutumia mifumo hiyo.

Mrajis Ndiege amefafanua kuwa manufaa ya mfumo huo ni mkubwa ambapo mwaka huu ambao umeishia Juni ndio wameanza kuutumia na tayari wamesajili vyama 6000 ndani ya mfumo kati ya vyama 7300.

Ameeleza kuwa tayari wameshapata takwimu ya vyama hivyo na  wanachama wao wameanza kutambulika kutokana na mfumo huo kutambua chama na wamachama wake.

Ameeleza kuwa Vyama hivyo tayari vimeshaanza kutumia mfumo  huku akitolea mfano kabla ya mwaka kuanza vyama  vinatakiwa kupitisha bajeti zao katika ofisi ya Mrajis ambapo vyama vimeshaanza kupitisha bajeti hizo.

"Badala ya chama kusafiri kutoka kwenye ofisi zake  kwenda katika ofisi ya Mrajis wa Mkoa au kwenda kwenye ofisi ya Mrajis Taifa ana apulodi taarifa zake kwenye mfumo na zinapitiahwa na Mrajis hata ile gharama ya kusafiri inakuwa haipo," amesema.

Amesema kwenye mfumo huo tayari wameshaanza kutoa leseni ya vyama vya akiba na mkopo (SACCOS), kwa mujibu wa sheria ya huduma ndogo  za fedha wote wanatakiwa kuwa na leseni ya kufanyia kazi hivyo zinaomba leseni kupitia Mfumo huo.

Mrajis huyo amesema tayari SACCOS zimeshaanza kupeleka taarifa zake kupitia mfumo huo na wameshaanza kuzikagua na kuzisimamia kwa kupitia taarifa hizo ambazo zimeingia kwenye mfumo huo.

Amefafanua kuwa walikuwa na kazi kubwa ya kufanya uelimishaji kuhusu mfumo huo sio wote ambao wanaweza kuutumia hivyo vyama vingi watendaji wake walikuwa hawana elimu ya kutosha.

Kwa mujibu wa Mrajis huyo mwaka uliopita wamefanya kazi ya kuwaelimisha na kuwaonesha namna ambavyo watautumia mfumo huo.

Amesema kuna vyama ambavyo vilikuwa haina vitendea kazi kwa sasa wanahamasisha vyama ambavyo haijawa na miundombinu ya kutosha viweze kununua.

Mrajis huyo amesema mikakati ya Tume hiyo ni kuhakikisha Watanzania wengi wanatumia mfumo huo kwenye shughuli zao za kila siku.

Amesema mkakati mwingine wa Tume hiyo ni kuwa na vyama vya ushirika ambavyo ni imara zaidi na vinafanya kazi kisasa na malengo ya kibiashara.

Post a Comment

0 Comments

DKT. BITEKO ASISITIZA UMUHIMU WA MIFUMO THABITI YA NISHATI JADIDIFU KUKIDHI MAHITAJI YA NISHATI