WATOTO 2300 WAMEOKOLEWA AJIRA ZA TUMBAKU


Na Asha Mwakyonde, Mbeya

ZAIDI ya watoto 2300 wameokolewa kutoka katika shughuli za uzalishaji wa zao la  tumbaku ambazo ni hatarishi kwao na wengine kupatiwa elimu ya ujasiriamali, mafunzo stadi ambapo kwa sasa wanafanya shughuli zao nyingine.

Hayo yamesemwa jijini Mbeya leo 5, 2023, na Meneja  Mradi wa  Prosper Reset kutoka mkoani Tabora  Fredrick Malaso katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', amesema kuwa wamevuka lengo  walilokusudia la  kuwafikia watoto 2200 hadi sasa wamewafikia watoto 2300.

Amesema baadhi yao waliomaliza shule wameingizwa katika shughuli mbadala ambapo kwa  sasa  hawajihusishi na shughuli za uzalishaji wa tumbaku ambazo ni hatarishi kwao.

Malaso amesema wapo wanaoendelea lakini tayari wamepatiwa elimu ya kuzalisha tumbaku kwa kuzingatia utaratibu na mifumo maalumu ya kuzingatia afya zao.

Amefafanua kuwa mradi huo umejikita katika kuwajengea uwezo jamii wa kuinua uchumi wa familia ambazo zipo vijijini zinazojihusisha na shughuli za uzalishaji wa tumbaku.

"Tunatoa elimu ili wazazi wasiwatumikishe watoto katika shughuli za uzalishaji wa tumbaku tunawapatia elimu ya kufanya shughuli mbadala za kuongeza kipato ili kuhakikisha watoto wanapata fursa yao ya kupata elimu na kucheza," amesema 

Ameongeza kuwa kupitia fursa wanazozipata wazazi wanawapatia huduma za msingi watoto wao ikiwamo afya na kuwasaidia kuwapatia vifaa vya shule.

Malaso ameeleza kuwa awali mradi huo ulikuwa unawasaidia wazazi kuwapatia madaftari na vitabu ambapo kwa sasa wanawajengea uwezo wazazi hao ili yale mahitaji ya msingi ya watoto waweze kuwajibika wenyewe na kuhakikisha wanawasimamia na hawawatumikishi katika shughuli hatarishi za uzalishaji wa tumbaku.

Amefafanua kuwa wamechagua maeneo hayo kwa kuwa wadhamini wa mradi huo ni kampuni ya tumbaku.

"Maeneo ya Kaliua,Urambo na Sikonge kwa Tanzania ni maeneo ambayo ni makubwa yanayozalisha tumbaku na kwa upande wa Mbeya na Songwe wanazalisha tumbaku ndio maana tumejikita katika kusimamia jamii kuhakikisha inaepukana na vitendo vya utumikishaji wa watoto kwenye mashamba ya uzalishaji wa zao hili, " amesema.

Meneja huyo amesema mradi huo ulianza mwaka 2011 na unatarajiwa kumalizika hivi karibuni  unatekelezwa katika mikoa ya Tabora ambao unatekelezwa katika Halmashauri tatu ambazo ni Kaliua, Sikonge na Urambo, wilaya ya Songwe mkoani Songwe na Mbeya wilaya ya Chunya.

"Tumevuka lengo kutokana na mazingira pamoja na uhamashishaji baada ya kuwashirikisha wadau wengine mafanikio ni makubwa hata akina mama wengi wamejihusisha katika vikundi vya kuweka na kukopa," amesema.

Naye Afisa Elimu kazi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Honesta Ngolly amesema kuwa wanasimamia sheria za kazi nchini.

Amesema kuwa ofisi hiyo imeshiriki maonesho hayo lengo likiwa ni kukutana na wananchi kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa kwa kuwaelimisha wafanyakazi kuzingatia sheria kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuchumi, kuwa watulivu na kuweza kupata stahiki zao na kubuni mifumo mingine endelevu ya uzalishaji wa ajira na chakula nchini.

Ngolly amesema sekta ya kilimo imezalisha ajira nyingi nchini lakini kuna changamoto ndogo ya wafanyakazi waajiri kuwaajiri watoto chini ya umri wa mika 18 na wengine chini ya miaka 14.


"Kwa mujibu wa sheria ya ajira mahusiano kazini sura namba 366 kifungu cha 5 kinazuia ajira za mtoto, mtoto chini ya umri wa miaka 18 haruhusiwi kuajiriwa isipokuwa mtoto kati ya miaka 14 hadi 17 anaweza kupewa kazi ambazo zinamuandaa kupata ujuzi wa aina mbalimbali na hazipaswi kuwa na madhara kiafya, kielimu na mengine," ameongeza.

"Tupo hapa tumekutana na wakulima, Wafugaji wengi na Kampuni nyingi za ununuzi wa mazao hapa nchini,zinazofanya mifumo mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa mazao," amesema.

Afisa huyo amesema sekta ya kilimo ndio inayoongoza katika ukuzaji wa uchumi wa nchi hivyo wanashirikiana na serikali kuhakikisha sekta hiyo inakuwa Imara na haina migogoro mingi ili kuweza kuzalisha ajira zaidi.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU