HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAWEKA MKAKATI KUEPUKA BIASHARA YA FIGO


Na Asha Mwakyonde,Mbeya

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH),imesema kuwa wenza wanaweza kutoleana figo baada ya bodi ya idhini  pamoja na wadau tofauti tofauti kukaa na kuchunguza kwa kipindi cha wiki sita ili kubaini ukweli wa wenza hao lengo likiwa ni kuepuka biashara ya kuuziana figo.

Akizingumza  jijini Mbeya leo 5,2023, katika banda la hospitali hiyo
Mratibu wa Huduma za Upandikizaji Figo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Awadhi Mohamed, kwenye  maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', amesema wenza  wanatakiwa wawe katika ndoa ambayo inatambulika, iwe ya kidini au ya Serikali.

Amefafanua kuwa  mchakato huo hupita katika ngazi tofauti na kuidhinishwa na bodi ya idhini ambayo hukutanisha wataalam, watu kutoka sekta tofauti kuhakikisha ulikuwa sahihi na wa haki na ulifuata masharti na vigezo vyote.

Ameeleza kuwa kuna taratibu ambazo zinatakiwa kufuatwa kabla ya mtu kutolewa figo ikiwemo kutambua kama mgonjwa husika anaweza kupandikizwa kwa vigezo vya kiafya, kijamii na kisheria na kupata mchangiaji anayetoka katika ndugu.

"Dunia iliweka tahadhari hii na watu wakakutana na kusema kama hakuwa na sheria nzuri na utaratibu mzuri uchangiaji ufanyike kwa watu wa karibu wenye uhusiano lengo ni kuepuka watu wasiingie katika biashara ya viungo," amesema.

Mratibu huyo amesema kuwa miongo kadhaa iliyopita dunia ilishuhudia biashara ya viungo vya binadamu na kwamba ili kuweza kupunguza hilo kwa nchi kama Tanzania ambayo bado haina sheria za kusimamia Uratibu  wa uchangiaji wa viungo lazima kuwe na tahadhari.

Mratibu huyo amesema kuwa hakuna Taifa lolote duniani ambalo limeruhusu mtu kuuza kiungo chake kumpa mtu mwingine.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI