TUFANYE KAZI KWA USHIRIKIANO ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI.

Na WAF, Dodoma.

WAZIRI wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka watendaji ndani ya Sekta ya Afya kufanya kazi kwa ushirikiano na kuleta tija katika kuboresha ubora wa huduma za afya nchini.

Waziri Ummy amesema hayo leo Septemba 5, 2023 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Watumishi wa Wizara ya Afya kuhusu mipango ya utekelezaji wa afua za kufikia vipaumbele 14 ambavyo vimewekwa na Wizara ya Afya kwenye Bajeti ya mwaka 2023/24.

“Dhamira  yangu ni kuboresha ubora wa huduma za afya nchini, tufanye kazi kwa ushirikiano na kuweka mbele masilahi ya Sekta ya Afya na Tanzania,” amesema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy amesisitiza watendaji ndani ya Sekta ya Afya kuijua vyema Sekta na kufanya mambo yenye tija katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Amesema kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika kuboresha Sekta ya Afya nchini kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za Afya, ununuzi wa dawa, vifaa na vifaatiba, ajira za watumishi pamoja na kusomesha wataalam, hivyo ni wajibu wa watendaji ndani ya Sekta ya Afya kuhakikisha wanaboresha huduma za afya wanazotoa kwa wananchi.

“Sekta ya Afya ina fedha nyingi na wadau wengi wanaofanya kazi, naomba tuelekeze fedha hizo katika kuboresha huduma za Afya ili wananchi waweze kunufaika na upatikanaji wa huduma bora za Afya”, amesisitiza Waziri Ummy.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesisitiza watendaji ndani ya Wizara na Sekta ya Afya kwa ujumla kufanya kazi kwa umoja na kushirikiana katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Dkt. Jingu amesema kuwa watendaji wana dhamana kubwa ya kutatua kero za wananchi hivyo ushirikiano wa karibu katika kuhudumia wananchi utaleta tija katika uboreshaji wa huduma za Afya nchini.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU